Uchungu wa mama: Mama azungumzia kuuawa kwa mawanawe na polisi

MAMA LUCY HOSP
MAMA LUCY HOSP
"Mama hafai kumzika mwanawe, ni mtoto anayestahili kumzika mamake akiwa mzee, yauma sana, hasa ikiwa mwanao ameuawa kinyama.”

Haya yalikuwa matamshi ya mama Sarah Wangari ambaye mwanawe wa kiume alipigwa risasi na kuawa na afisa wa polisi. Sarah alinyamaza na kupanguza machozi.

"Nilikuwa mama Daddy, lakini sasa naitwa tu Sarah Wangari."

Daniel Mburu alipigwa risasi na afisa wa polisi alipokuwa amekimbiza mtoto wa jirani katika hospitali ya Mama Lucy. Mburu ambaye alikuwa mhudumu wa bodaboda mwenye umri wa miaka 24, aliishi karibu na mamake mtaani Korogocho. Alikuwa kazini kama kawaida alipopokea ujumbe kwamba mtoto wa jirani aliyekuwa karibu afe maji alihitaji kukimbizwa hospitalini. Alijitolea kumpeleka mtoto huyo katika hospitali ya Mama Lucy Kibaki na kuambia jirani amweleze mamake alikokuwa ameenda.

“Alikuja kuniaga lakini hakunipata. Mara ya mwisho nilimuona ilikuwa siku ya Jumapili. Alikuwa mkakamavu na kuomba chai kasha akaondoka,” Sarah alisema.

Kennedy Kimani, aliyekuwa ameandamana naye hospitalini alishuhudia tukio hilo, alisema marehemu alikuwa ameacha pikipiki karibu na lango na kumbea mtoto aliyekuwa katika hali mbaya ndani ya hospitali kitengo cha dharura.

Waliambiwa na madaktari kutoka nje ili mtoto huyo ahudumiwe. Walipokuwa wanatoka nje alimuona Mburu akienda kuchukuwa pikipiki yake. Muda mfupi baadaye malumbano yalizuka na polisi akampiga kofi Mburu.

"Nilisonga karibu kuona nini kilikuwa kinaendelea. Afisa huyo alikuwa anamuuliza kwanini alikuwa ameegesha pikipiki karibu na lango kuu" Kimani alisema.

Rafiki yake mwingine alikimbia kumtetea Mburu, lakini pia yeye alipigwa rungu na polisi. Wawili hao waliwekwa pingu pamoja na kupelekwa katika chumba cha walinzi na kuacha watu wakiandamana.

"Afisa huyo alitayarisha bunduki na umati wa watu ukasalia mbali kwa hofu. Aliondoka na wawili hao na muda mfupi baadaye tukasikia mlio wa risasi," Kimani alieleza.

Alisema watu walikimbia mahali Mburu na wenzake walikuwa wamezuiliwa kuona nini kilikuwa kimetendeka. Mburu alikuwa amepigwa risasi kifuani.

"Niliona walinzi wanne wakimvuta kuelekea eneo la wagonjwa mahututi. Wakati huo watu wengi walikuwa wameanza kupiga mayowe wakipinga tukio hilo," alisema.

Mamake Mburu alisema kwamba aliporejea kutoka madukani, alisikia wahudumu wa bodaboda wakipiga honi na kelele.

"Nilifikiri yule mtoto amefariki. Nakumbuka nikisema kimoyo moyo huzuni ambayo mamake anahisi," Mamake Mburu alisema.

Wangari alisema rafikiye mwanawe Mburu alimwambia apande kwa pikipiki waelekea hospitalini.

"Nilipanda kwa pikipiki. Muda huu wote sikujua mwanangu ameuawa, hakustahili kufariki,” alisema.

Akiwa hospitalini, rafikiye Mburu alimwambia kwamba mwanawe wa pekee alikuwa amepigwa risasi na afisa wa polisi.

“Nilikimbia na kupata madaktari wamemzingira. Niliambiwa nisubiri huku wakijaribu kuokoa maisha yake, lakini muda mfupi baadaye alikuwa amefariki. Niliona damu yake mahali alikuwa amezuiliwa. Nini kinafanyika katika nchi hii?” aliuliza.

Jamaa aliyeshikwa na Mburu aliachiliwa na kuonywa dhidi ya kusema lolote.

"Polisi alimtishia, akisema kwamba ‘nimekuachilia ukiwa hai, ukitoka hapa, hunijui na sikujui, ukisema chochote jilaumu mwenyewe,” Wainaina alisema.