Vipimo
Amesema Dr Njue, aliyekuwa ameandamana na wanafunzi kutoka chuo cha Kings Medical College, alinakili kwamba kifo cha Karau kilisababishwa na mshtuko wa moyo kwa ajili ya uvimbe katika mshipa wa damu ,lakini akasisitiza kwamba atauchukua moyo huo ili kuufanyia vipimo na kuthibitisha kikamilifu matokeo hayo .Dr Kimani amesema mwanzoni alihofishwa kwamba Dr Njue alikuwa akivibeba viungo hivyo kutoka kwa marehemu bila ruhusa ya familia yake lakini akajiambia labda Njue angewaeleza jamaa za marehemu baadaye . Ameiambia mahakama kwamba ingawaje mzee Karau alikuwa na majeraha yanayoonekana ,hayakuzingatiwa kama sababu ya kifo cha mzee huyo aliyekuwa na umri wa miaka 70.
Kabla ya kesi kuanza kusikizwa siku ya jumanne Bi.Martha Gokou alitaka kesi hiyo kuahirishwa ili wakili wake afahamishwe kuhusu suala hilo akisema kwamba alikuwa ametajwa pakubwa katika uchunguzi huo. Hata hivyo upande wa mashtaka ulifaulu kukataa ombi lake kwani mashahidi saba tayari walikuwa wamefika mbele ya jopo la uchunguzi kutoa ushahidi wao na Bi Gokou hakuonyesha nia yoyote ya kutaka kumhusisha wakili wake . Wakili wa serikali Anthony Musyoka pia amesema kwamba mahakama haijatoa uamuzi wa iwapo inafaa kumshtaki yeyote kuhusu kifo cha mzee Karau .
Sumu
Dr Kimani pia amesema walituma sampuli kwa mwanakemia wa serikali ili kufahamu iwapo mwendazake alipewa sumu . Ilikuwa ni baada ya familia kupitia wakili Charles Mwongela, kupata ruhusa ya kuufukua mwili wa marehemu ili uchunguzi wa pili wa kubaini sababu ya kifo chake kufanywa ndipo walipomuuliza Dr.Njue kurejesha moyo wa marehemu lakini Njue akazidi kukwepa .Dr Njue tayari ameshtakiwa kwa madai ya wizi wa viungo hivyo na uharibifu wa ushahidi .
Familia inadai kwamba kuondolewa kwa moyo na figo za marehemu ilikuwa njama ya kuficha ukweli kuhusu kilichosababisha kifo chake . Familia hiyo ilishauriwa na mtaalam kwamba majeraha ya kichwa yanaweza kusababisha kifo cha mtu wa umri wa juu na walitaka kuona endapo kulikuwa na majeraha katika mwili wa marehemu kuonyesha iwapo alijaribu kujikinga alipokuwa akishambuliwa na mtu . Vikao hivyo vitaendelea Agosti Mosi .