Uhuru amteua Ukur Yatani kaimu waziri wa fedha

ukur
ukur
Rais Uhuru Kenyatta amemteua waziri wa Leba Ukur Yatani kuwa kaimu waziri wa Fedha kuchukuwa nafasi ya Henry Rotich anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi.

Katika mabadiliko yaliotangazwa Jumatano alasiri Rais Kenyatta pia ameteua Dkt. Julius Monzi Muia kama katibu wa kudumu wa fedha kuchukuwa nafasi ya Kamau Thugge ambaye pia anakabiliwa na mashtaka ya ulaji rushwa. Hadi kuteuliwa kwake Muia alikuwa katibu wa kudumu katika wizara ya mipango ya kitaifa.

Torome Saitoti atahudumu kama katibu wa kudumu wa mipango ya kitaifa huku Meja Jenerali Gordon Kihalangwa akihamishwa wizara ya uhamiaji hadi wizara ya Ulinzi katika wadhifa wa katibu wa kudumu.

Rotich na Thugge walifikishwa mahakani siku ya Jummane na kushtakiwa kuhusiana na sakata ya ujenzi wa mabwawa ya Kimwarer na Arror.  Waliachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni 15 kila mmoja.