Uhuru asikitikia ajali za barabarani nchini

Rais Kenyatta ameelezea masikitiko yake kuhusiana na viwango vya ajali za barabarani nchini licha ya juhudi za serikali kugeuza muundomsingi wa barabara nchini.

Rais alisema wakenya wanaendelea kupoteza maisha yao na wengine kulemazwa kutokana na ajali za barabarani. Alikuwa akizungumza Siku ya Jumapili katika Ikulu ya Nairobi alipoongoza ukaguzi wa gwaride ya 91 ya kila mwaka ya shirika la St. John’s Ambulance iliyohudhuriwa na washirika 3,500.

Rais Kenyatta alitoa msaada wa shilingi milioni 10 kutambua juhudi za shirika hilo katika kuitikia visa vya dharura.  Rais alitoa wito kwa kiongozi anayeondoka wa shirika hilo Meja Mstaafu Marsden Madoka kumpa orodha ya wafanyikazi wa shirika hilo wanaoweza kutunukiwa tuzo za kitaifa kama motisha.

Madoka alipongeza serikali ya kitaifa na za kaunti kwa kushirikiana na shirika hilo kupunguza dhiki kwa wakenya. Waziri wa Afya Sicily Kariuki alisema pendekezo la mpango wa ushirikiano kati ya shirika hilo na wizara yake unaendelea kukamilishwa kabla ya kuwasilishwa kwa Rais katika kipindi cha siku 14.

Wakati huo huo, Rais alikubali ombi la shirika hilo kuanzisha kituo cha kushughulikia manusura wa ajali kwa ushirikiano na Wizara ya Afya ili kuhudumia vyema wakenya walioathiriwa na ajali za barabarani.  Alipongeza shirika la St John’s Ambulance kwa kusaidiana na serikali kufanikisha Ajenda Kuu ya Nguzo Nne za Maendeleo hasa katika afya kupitia kwa utoaji wa huduma za ambulansi na nyingineo.