Uhuru atakiwa kukataa kuidhinisha mswada wa kuongezea wabunge wa zamani pensheni

Mashirika matatu ya uajibikiaji wa raslimali za umma yamemtaka rais Uhuru Kenyatta kukataa mswada unaopendekeza wabunge wa zamani kulipwa pensheni ya shilingi laki moja kila mwezi.

Mashirika ya Transparency International, Muungano wa walipa ushuru na Taasisi ya uajibikaji wa jamii ( Social Accountability) yalisema kwamba ikiwa mswada huo utatekelezwa basi utakuwa na athari kubwa kwa gharama ya pensheni kwa serikali.

Soma habari zaidi;

Mashirika hayo yanataka mapendekezo ya kufanyia marekebisho ya pensheni za wabunge kuwasilishwa kwa tume ya kitaifa ya kudhibiti mishahara - SRC.

“Tungependa kuelezea kutoridhishwa kwetu na mswada huu ambao unalenga kupuuza jukumu la tume ya SRC kama ilivyo katika katiba,” mashirika hayo yalisema katika taarifa ya pamoja siku ya Ijumaa.

Waliongeza, “Tunamkumbusha rais na viongozi wengine nchini Kenya kwamba wafanyikazi wa serikali wanawakilisha asilimia 17 pekee ya wananchi wa Kenya. Kwa hivyo majaribio ya kutaka kuwapa malipo ya juu zaidi huku wakenya wengine wakiumia yanafaa kukataliwa mbali.”

Walisema kwamba hata kama rais anahimiza vijana kujifunza masomo ya kiufundi na kujiajiri, sera za serikali zinafaa pia kulenga kufanikisha azimio hili.

Soma habari zaidi;

“Ushuru ambao utafadhili pensheni hizi utatolewa na wafanyikazi wote wakiwemo wale wa sekta za juakali, sio haki kugawia sekta moja pekee faida ya ushuru unaolipwa na sekta zote,” walisema.

Tume ya SRC ndiyo taasisi ya pekee iliyopewa jukumu la kudhibiti mishahara na marupurupu mengine ya wafanyikazi wa serikali.

Kuna hofu kuwa nyongeza ya pensheni ya wabunge huenda ikachochea wafanyikazi wengine wa umma kudai malipo ya juu ya uzeeni.

Soma habari zaidi;

Bunge la kitaifa wiki iliyopita liliidhinisha marekebisho kwa mswada wa 2019 kuwatunuku takriban wabunge wa zamani 375 pensheni ya shilingi laki moja kila mwezi. Watakaonufaika ni wabunge waliohudumu kati ya mwaka 1984-2001.