Uhuru: Sina nia ya kuongeza muda wangu madarakani

Rais Uhuru Kenyatta ameshikilia kwamba hana nia ya kusalia madarakani kwa kuzidisha muda wake afisini kupitia kura ya maoni.

Uhuru  amesema katiba ipo wazi kuhusu muda wa kuhudumu kwa anayeshikilia wadhfa  wa urais. Ameongeza pia kwamba hana lengo la kuwa  waziri  mkuu kama inavyodaiwa.

Uhuru  alikuwa akiyajibu maswali ya Katrina Manson  wakati wa mkutano uliofanywa kwa njia ya video  na  Atlantic Council.

Uhuru  alisema, “ iwapo kuna kitu ambacho wakenya wanakifahamu kwa uwazi kabisa ni kuhusu  mihula miwili ya kuhudumu kama rais. Hilo limekuwa wazi tangu mwaka wa 1992 tulipoanzisha  mfumo wa siasa za vyama vingi  na hakuna rais ambaye amewahi kuvunja hilo nchini na kamwe sitaki kuwa wa kwanza kufanya hivyo’

Uhuru  amesema lengo la mwafaka wa BBI ni kuhakikisha kwamba vizazi vijavyo havikumbani na changamoto zinazolikabili taifa kwa sasa.

" Sina  ufahamu wa iwapo kutakuwa na wadhifa wa waziri mkuu katika katiba, Haya sio  maswali  ambayo watu wameanza kuuliza. Nimekupa  mtiririko wa yote ambayo wakenya wanataka  yashughulikiwe kama vile nguvu ya kura zao,   ugavi wa  raslimali na kujumuishwa serikalini’.

Uhuru amesema kando na hayo hajasikia kuhusu masuala mengine yanayoibuliwa na hivyo basi hawezi kuyazungumzia  kwani hayamo katika msingi wa BBI