Ukanda unaomuonyesha Babu akimpiga DJ Evolve risasi waweza kutumika mahakamani

Ukanda wa CCTV unaomuonyesha mbunge Babu Owino akimpiga risasi mcheza mziki au DJ katika klabu moja huko Kilimani unaweza kutumika kama ushahidi wa kielektroniki, mahakamani.

Wakili Boniface Oduor hata hivyo anasema ni lazima klabu hio ipate cheti cha ushahidi wa kielektroniki ili ukanda huo uweze kukubalika.

Owino alilala kizuizini katika kituo cha polisi cha Kilimani kuhusiana na kisa hicho cha hapo jana. Mkuu wa polisi wa Kilimani Lucas Ogara anasema bunduki iliyotumiwa imenaswa huku uchunguzi ukiendelea.

Hayo yakijiri, wasanii sasa wataweza kufuatilia iwapo kazi zao zimepeperushwa kwenye runinga au redioni, kwa minajili ya kuhakikisha wanalipwa pesa zifaazo. Mwenyekiti wa shirika la kutetea haki zao Ephantus Kamau anasema wanaweka mfumo wa kiteknolojia wa kuweza kufuatilia hilo.

Kwinginkeo, mashambulizi ya mara kwa mara na majangili huko Kapedo yameilazimu serikali kutumia kima cha shilingi milioni 24 kujenga kuta katika shule mbali mbali zinazoathirika kutokana na mashambulizi hayo ili kuwapa mazingira  yaliyo salama ya kuendeleza masomo. Eneo hilo la Kapedo linakabiliwa na wizi wa mifugo na migogoro baina ya jamii za Pokot na turkana.

Katika taarifa za tanzia, Jaji mstaafu Daniel Aganyanya amefariki dunia. Inaarifiwa kuwa alifariki jana jioni katika hospitali mjini Kisumu ambapo alikua amepelekwa baada ya kupatwa na matatizo ya kupumua, akiwa nyumbani kwake huko Hamisi, kaunti ya Busia.

Aganyanya ni mumewe jaji Roselyn Nambuye.