Ukatili wa polisi! Mahakama yaelezwa vile Wakili Willy Kimani aliuawa kinyama na polisi

jaji
jaji
Mahakama siku ya Jumatatu ilielezwa kwa utaratibu vile wakili Willy Kimani aliuawa kinyama na maafisa wa police.

Ni hadithi ya njama, udanganyifu na kutoelewana iliopelekea mahakama kueleza kilochotokea wakati wa kuuliwa kwa watu waliokamatwa kwanza kama wahalifu. Afisa wa polisi Geofrey Kinyua alisimama kizimbani kusoma ushahidi wa jamaa aliyekubali kutoa habari kwa upande wa mashtaka, Peter Ngugi kuhusu vile wanaume watatu waliuawa na maafisa wa polisi. Peter Ngugi pia ni mmoja wa washtakiwa katika mauaji hayo.

Ushahidi huo uliotoa taswira ya unyama aliotendewa wakili Willy Kimani na wanaume wengine wawili kabla ya kuuawa uliwaacha wengi mahakamani wakiwa vinywa wazi. Wengine wawili waliouawa ni dereva wa teksi Joseph Muiruri na mteja wa wakili Kimani, Josphat Mwenda.

Ngugi, aliyekuwa mhudumu wa bodaboda alichukuliwa na polisi ili awasaidie kupata habari muhimu kuhusu mauaji ya watatu hao.

Ngugi alifichua vile waliua Kimani na watu wengine wawili kabla ya miili yao kutupwa katika Mto Donyo Sabuk. Kazi yake ilikuwa kuondoa wahasiriwa kutoka buti la gari na kuwakabidhi polisi kuwaua. Saa nne usiku, mhudumu wa bodaboda, Mwenda alikuwa wa kwanza kumalizwa kwa kunyongwa kwa kamba.

Saa moja baadaye, mhasiriwa wa pili, Muiruri alipelekwa pembeni na kuuliwa kwa kunyongwa na kisha kuwekwa ndani ya magunia mawili kwa sababu alikuwa mrefu na hangetoshea katika gunia moja.  Mhasiriwa wa tatu wakili Willy Kimani pia aliuliwa kwa kunyongwa na mwili wake uliwekwa kwa gunia kando ya mwili wa mhudumu wa bodaboda.

Kisha, Ngugi aliendesha gari na miili miwili huku Kamenchu akiongoza msafara na mwili wa tatu kuelekea mto Ol Donyo Sabuk. "Tulifika mtoni na kuondoa mwili wa kwanza na kuutupa mtoni,” Ngugi alisema katika ushahidi wake.

Aliongeza kuwa walisonga mbele mita chache na kutupa miili mingine miwili. Baada ya kutupa miili hiyo, walirejea Mlolongo mwendo wa saa kumi asubuhi na kupata chakula katika baa moja mjini humo kabla ya kila mmoja kwenda zake lakini Ngugi alisalia.

Ngugi pia alieleza matukio yaliyotendeka kabla ya siku ya kuuawa kwa watatu hao. Matukio yalianza kwa yeye kuwafuata wahasiriwa. Katika ushahidi wake anasema kwamba, Mwezi Aprili mwaka 2016, afisa wa polisi kutoka kituo cha Kabete alimuita na kumweleza kwamba alikuwa amehamishwa kutoka Busia hadi Mlolongo.

Aliongeza kwamba alipoenda kumtembelea hapo ndipo alipokutana na Sajenti Fredrick Ole Leliman, ambaye pia ni mshukiwa katika kesi hii. Ni wakati huu ambapo Leliman alimwambia kwamba alihitaji usaidizi wake akisema kwamba alikuwa amempiga risasi na kumjeruhi mwendesha pikipiki na kutokana na tukio hilo jamaa aliyepigwa risasi alitaka afutwe kazi.

Leliman alimfichulia kwamba huyo bodaboda alikuwa anasaidiwa na IPOA na kwamba kesi ilikuwa mahakamani na alitaka waivuruge. Ngugi alisema kwamba mpango ulikuwa kumuua mhudumu wa bodaboda na kazi yake ilikuwa kumfuata na kupiga ripoti kwa Liliman kuhusu pitapita zake.

Anasema, alikutana na Leliman akiwa na mwanamke mmoja Juni tarehe 23, 2016 eneo la Mlolongo na mwanamke huyo akaahidi kumwonyesha jamaa aliyelengwa. Leliman kisha aliwaachia shilingi elfu mbili ili wagawane.

“Mwanamke huyo alionionyesha mhasiriwa na nikamtambua kabla ya mwanamke huyo kuondoka, simkumbuki mwanamke huyo, na tangu siku hiyo sijawahi kumwona tena,” Ngugi alisema katika ushahidi wake.

Ngugi alimfuata bodoboda huyo mahakamani. Kesi siku hiyo ilichukua takriban saa mbili.

Kesi ilipokamilika, jamaa huyo alitoka nje lakini alikuwa na mtu mwingine. Kisha alimpigia simu Leliman aliyemwambia kwamba huyo mtu mwingine pia alikuwa mwizi. Wawili hao waliingia katika gari moja na Ngugi naye akaenda katika gari lake Leliman na kumpata Sergent Mwangi.

Gari lililokuwa na jamaa wa boda aliyekuwa analengwa lilipita na kisha Leliman akalifuata.

“Tuliwapata katika Railway Station na Mwangi akatoa Walkie talkie yake na kuwaambia kwamba alikuwa chini ya mikono ya polisi. Hawakupingana. Waliingizwa kwa gari la Leliman na kupelekwa katika kambi ya AP.

Ngugi alisema kwamba kazi yake pia ilikuwa kutupa gari walimokuwa watatu hao.

Mpango ulikuwa kulipeleka gari hilo mjini Meru, lakini Leliman alionya kwamba lilikuwa likihudumu kama teksi katika eneo la Zimmerman na ingekuwa hatari kutumia barabara hiyo.

Mwendo wa saa moja jioni Leliman alipigiwa simu na kuarifiwa kwamba mmoja wa watatu hao alikuwa amempigia mkewe simu kumuarifu kukamatwa kwao.

Walirejea kituoni na Leliman akawachukuwa watatu hao na kuwaweka ndani ya buti la gari lake wakiwa na pingu mikononi.

"Kutoka hapo tuliendesha gari hadi kichakani, tulianza kutofautiana namna ya kuwaangamiza watatu hao," Ngugi alisema katika ushahidi wake.

Aliongeza kuwa ; "Mimi na afisa mwingine tulitaka watatu hao kuachiliwa kwa sababu tayari njama yao ilikuwa imetambulika na tayari walikuwa wamepelekwa hata katika kambi ya polisi. Hata hivyo, Leliman alisisitiza kuwa lazima wauwawe."

Ngugi anasema kwamba walibishana kwa tabriban saa tatu kuhusu nini wangefanya.