Ukienda wanakochoma nguruwe unakuta vijana wamejaa - Museveni

nguruwe
nguruwe

Rais Yoweri Museveni amewataka vijana kufuata na kulinda utamaduni wa Kiafrika na sio kudanganywa na ulimwengu wa kimagharibi ambao ameuelezea kama "unaoumwa'', limeripoti gazeti la Daily Monitor nchini humo.

"Nchi za magharibi hazina miwani ya kuona utofauti kati ya mwanamke na mwanamme . Ni wagonjwa . Urithi wa utamaduni wetu lazima udumishwe, lakini wengine utamaduni wetu unaofuatwa na 68% ya watu , ubadilishwe kwa lazima ," amesema Bwana Museveni.

Rais huyo wa Uganda ametoa kauli hizi alipokuwa akikutana na wawakilishi wa vijana kutoka maeneo mbali mbali ya nchi hiyo wanaounda baraza la kitaifa la vijana- National Youth Council katika Wilaya ya Jinja Jumatano.

Bwana Museveni amewashauri vijana juu ya kile alichokiita "nidhamu ya jamii" kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na sherehe kubwa na anasa. Amesema pia anashangazwa ni pesa gani vijana wanazimwaga kwenye baa huku wakidai hawana pesa.

"Unaenda baa unawakuta wamejaa, ukienda wanakochoma nguruwe unakuta vijana wamejaa. Huu ni utovu wa nidhamu ya jamii na ni sehemu ya tatizo tunalokabiliana nalo ," anasema Museveni.

Katika taarifa iliyotolewa na maafisa wake wa habari , Bwana Museveni alisisitizia umuhimu wa haja ya kuwa na nidhamu ya kiuchumi na akaahidi usaidizi wa serikali yake kwa vijana ambao watafungua vyama vya ushirika na kujihusisha na shughuli za uzlishaji, limeripoti gazeti la Daily Monitor.

-BBC