'Ukikosana na mke lala nje! ' - Wana Jambo watoa maono

'Kila mtu ana siku yake ya kuzaliwa na kuzama kutoka duniani' aliimba msanii Jaguar. Ila vifo zingine hutokea kwenye mazingira tatanishi sana.

Mume amuua mke kwa kumdunga kisu, mpenzi ampiga bunduki mwenzake na baadae kujitoa uhai, mume ateketeza nyumba yake mke na watoto wake wakiwa ndani, bibi amuekea mume sumu na kumuua...

Watu kuuwawa kinyama imekuwa ni kama jambo la kawaida. Habari za vifo za hapa na pale zimetanda sana kwenye vyombo vya habari na kwenye mitandao za kijamii.

Hii leo kwenye kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi, mjadala ulikuwa kuhusu chanzo cha mauaji katika nchi yetu na jinsi ya kuyazuia. Baadhi ya wakenya walikuwa na haya ya kusema;

Kulingana na mzee Kobe, vifo vya sasa vimekuwa tisho sana kwani watu wanauawa kwa visu na bunduki kila siku. Aliwasihi wanaume wenzake waende kwenye sehemu za burudani kushusha hasira kukiwa na ugomvi nyumbani. Baada ya kushusha hasira inafaa warudi nyumbani na wakae chini wasuluhishe matatizo yao. Aliwaashauri pia wawe na mazoea ya kuwasiliana wakiwa na shida yoyote.

Mama Maria alisema;

"Zamani watu walikosa lakini mzee angeleta shida mke angeenda kwa jirani na kupitisha usiku mzima huko na kurudi baada ya hasira kupoa, mzee angewaita wazee wenzake ikiwa mama ameleta kisirani ili wasuluhishe tatizo."

Msikilizaji mwingine, Harun, alimuunga mzee Kobe mkono kwani alihisi ikiwa mtua anahasira na wamekorofishana na mpenzi wake anafaa achukue muda awe pekee yake ili ashushe mori.

Edward alichangia;

"Watu wataka suluhisho, ukikosana na mke ulale nje kisha urudi nyumbani, suluhu haijapatikana, nafsi hujaa kwa sababu ya kuweka hisia chungu kwa muda mrefu. Wazazi muwaingize watoto kanisani na muombe kama familia kila usiku."

'Wanandoa mnapokosana na kuna vitisho za kuuana au kuchapana, ombana msamaha na watu warudi kwa Mungu kwani ukiishi kwa upanga utakufa kwa upanga.' Alisema Kiderenge.

Tuwajibike sote kwa kusameheana na kuwasiliana muda kwa muda ili kutatua shida zetu za kifamilia bila kumwaga damu yoyote kwani hakuna mwanadamu mwenye haki ya kutoa maisha ya mwenzake.