Umeshuhudia upepo mkali hapo ulipo?

upepo
upepo
Idara ya utabiri wa hali ya anga imeonya juu ya upepo mkali unaotarajiwa kuvuma katika kaunti za Kiambu, Nairobi na Machakos na Kajiado kwa siku tano zijazo.

Upepo huo wenye kasi zaidi ya mita 20 kwa sekunde (20m / s) umeshuhudiwa katika maeneo mengi yakiwemo taifa jirani la Tanzania huku ukisababisha hasara nyingi sana pamoja na maafa.

Katika mahojiano ya kipekee na mkurugenzi msaidizi wa huduma ya hali ya anga Samwel Mwangi alithibitisha kuwa upepo mkali umeathiri mji wa Thika na kuangusha mabango barabarani.

"Upepo mkali utashuhudiwa Nairobi kote. Tayari upepo huo umeangusha mabango,"alisema.

Alishauri Wakenya waepuke kutembea karibu na mabango au chini ya miti.

Naye kaimu mkurugenzi wa idara ya hali ya anga, Stella Aura, alisema kuwa mvua kubwa zaidi ya 30mm inatarajiwa katika kaunti za Siaya, Kisumu, Homabay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia na Baringo katika siku tano zijazo.

Pia alisema mvua ya wastani inatarajiwa katika jiji la Nairobi na maeneo ya Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga na Murang'a.

Aidha Aura alitaka mipango na mikakati ya dharura ya kuzuia mizozo katika ukanda wa pwani na eneo la Kusini Mashariki kutokana na mzozo wa rasilimali chache.

"Hatua madhubuti zinafaa kuchukuliwa ili kukabili migogoro ya kila mara baina ya binadamu na wanyamapori kutokana na uchache wa rasilimali." alisema.