UPEKUZI: Mwalimu ndiye aliyepanga shambulizi la kigaidi Wajir

Maafisa wa usalama nchini Kenya wanasema mwalimu mmoja wa shule ya msingi ndiye aliyepanga an kuongoza shambulizi la kigaidi dhidi ya basi la abiria kaskazini mwa taifa hilo mwishoni mwa wiki.

Duru za kuaminika zilidokezea BBC kwamba mwalimu huyo wa kiume aliwahifadhi baadhi ya wapiganaji wa Al-Shabaab walioingia nchini Kenya wiki tatu zilizopita.

Maafisa saba wa polisi na daktari mmoja ni miongoni mwa watu 10 waliouawa kwenye shambulizi hilo.

Kwa mujibu wa gazeti la The Star, nchini Kenya, mwalimu huyo ametorokea taifa jirani la Somalia baada ya vikosi vya usalama vya Kenya kuanzisha msako mkali dhidi ya wanamgambo wa Al-Shabaab katika eneo la Wajir.

Afisa mmoja wa usalama aliambia BBC kwamba mwalimu huyo mkuu wa shule moja ya msingi katika eneo la Wajir aliongoza kundi la wapiganaji 15 kushmbulia basi jilo la abiria.

Polisi wanasema wamewatia mbaroni watuhumiwa 11 wa shambulio hilo la kigaidi akiwemo mke wa mwalimu huyo.

Maafisa saba wa polisi na daktari mmoja ni miongoni mwa watu 10 waliouawa katika shambulio hilo

Askari hao wamedaiwa kutoka katika kitengo cha Anti-stock huku utambulisho wa raia wengine wawili waliouawa ukiwa haujulikani.

Walioshuhudia waliiambia BBC kwamba wapiganaji kadhaa waliokuwa wamejihami walishambulia basi hilo lililokuwa likielekea Mandera na kuwalenga watu wasiotoka katika eneo hilo baada ya kuwatenga kutoka kwa abiria wengine.

Kisa hicho kinadaiwa kufanyika kati ya miji ya Wargadadud na Kutulo.

Kamanda wa polisi katika kaunti hiyo Stephen Ngetich alithibitisha tukio hilo.

''Naweza kuthibitisha kwamba kundi moja la watu waliojihami walishambulia basi ambalo lilikuwa linaelekea Mandera siku ya Ijumaa jioni'', alisema.

Basi hilo la Madina linadaiwa kushambuliwa mwendo wa saa kumi na moja jioni.

Shambulio hilo linajiri mwezi mmoja baada ya wapiganaji wa al-Shabab kushambulia kituo cha polisi cha Wajir katika jaribio la kutaka kuwaachilia huru washukiwa wawili wa ugaidi ambao walikuwa wanazuiliwa katika kituo hicho.

Kundi la wapiganaji wa al-Shabab nchini Somalia ambalo limekuwa likitekeleza mashambulio hayo mara kwa mara katika eneo hilo limekiri kutekeleza shambulio hilo likisema kuwa limewaua takriban watu 10.

Katika taarifa iliyochapishwa katika mojawapo ya tovuti zake, kundi hilo linasema limewalenga abiria wasiokuwa Waislamu katika basi hilo.

Kisa hiki kimetokea katika barabara ambayo takriban Wakenya 28 waliokuwa wakisubiri basi moja walishambuliwa na kuuawa miaka mitano iliyopita.

Barabara hiyo ipo karibu na mpaka wa Somalia.

Tutazidi kukupasha zaidi.

-BBC