Urithi wa mali ya Jonathan Moi, watoto 6 watambuliwa kama wanufaika

Jonathan+Moi
Jonathan+Moi
Wanawake wawili wameshinda raundi ya kwanza ya kesi inayohusiana na urithi wa mali ya marehemu Jonathan Moi, hii ni baada ya mahakama kutambua watoto wao kama miongoni mwa wale watakaonufaika.

Wanawake hao walikuwa wanataka mjane Sylvia kunyimwa madaraka ya kusimamia mali hiyo peke yake. Jonathan alikuwa mwanawe Rais mstaafu Daniel Moi.

Jaji Aggrey Muchelule aliamuru watoto hao 6 kutajwa kama wanufaika wa mali hiyo baada ya makubaliano baina ya pande zote mbili katika kesi hiyo.

 Watoto watatu ni wa Faith Mburu, huku wawili wakiwa wa Beatrice Mbuli. Mtoto wa sita alikuwa ameingia katika kesi hiyo kama mpingaji.

Jaji huyo pia aliagiza wahusika kukusanya na kuleta mahakamani orodha ya mali hiyo kwa wiki mbili zijazo.

Joshua Mutai pia aliruhusiwa kushiriki katika kesi hiyo kwa niaba ya wadai. Idhini hiyo ilitokea baada ya wanawake hao wawili pamoja na mutai kuwasilisha pingamizi.

Beatrice na Faith walisema kuwa walifunga ndoa kihalali na Jonathan Moi. Walimshtaki Sylvia kwa kudai kuwa ndiye mjane pekee wa Jonathan na kuenda kortini kutafuta barua za utawala huku akiwatenga.

Sylvia alikuwa ameiomba korti kumruhusu kusimamia mali hiyo kwa madhumuni ya kulipa kodi.

Kesi hiyo itatajwa mnano Desemba 11.