Usaliti ama ni siasa? Ruto atembea kwenye wembe wenye makali huku Uhuru akianza kuchukua udhibiti

uhuru 1
uhuru 1
Kilichoanza  kama vita baridi kati ya naibu wa rais William Ruto na mkuu wake rais Uhuru Kenyatta hatimaye kinajitokeza wazi- kufurushwa kwa washirika wa karibu wa Ruto kutoka nyadhifa muhimu katika bunge na pia serikalini .

Maelezo kuhusu mpango wa kenyatta kuchukua usukani wa seneti yameibuka siku chache tu baada ya chama cha Jubilee kufanya mkataba na kile cha Kanu kushirikiana katika serikali. Watakaoonyeshwa mlango ni seneta wa Elgeyo Marakwet  Kipchumba Murkomen na mwenzake wa Nakuru Susan Kihika wanaohudumu kama kiongozi wa wengi katika seneti na  kiranja wa waliowengi  mtawalia .

Kuingizwa serikali kwa Gideon Moi ni hatua inayolenga kumpa nafasi ya Ruto serikalini ambaye amejipata kutengwa katika serikali aliyosaidia kuundwa. Ruto na Gideon hawapatani na hilo limetumiwa kama chombo cha kumnasa mwanawe huyo wa Moi na kumtenga Ruto. Nduru zaarifu kuwa  Jubilee pia inalenga kufanya mkataba na chama cha Wiper cha Kalonzo Musyoka, hatua ambayo huenda ikalazimu mageuzi kufanywa katika baraza la mawaziri. Inaripotiwa Kalonzo mwenyewe anasisitiza kwamba awekwe katika baraza la mawaziri lakini hilo linapingwa na  baadhi ya wandani wa Jubilee. Mazungumzo kati ya rais Uhuru  na kiongozi wa ODM Raila Odinga yalitibuka baada ya Odinga kutaka kutengewa sehemu ya nyadhifa serikalini .

Rais Uhuru Kenyatta leo anatarajiwa kuongoza mkutano wa maseneta wa Jubilee ambapo mageuzi hayo yanatarajiwa kutekelezwa. Murkomen  ni kiongozi muhimu katika mipango ya Ruto ya kuwania urais mwaka wa 2022 na hatua yoyote ya kumpokonya nafasi yake katika seneti itakuwa pigo kwa azma aya Ruto. Kihika ni mshirika wa karibu wa Ruto na amekuwa nguzo muhimu sana katika kumuunganisha DP  na jamii ya kikuyu anapoendelea na kampeni za kutaka kumrithi rais Kenyatta .

Nduru zaarifu kuwa nafasi ya Murkomen huenda ikatwaliwa na  Gideon Moi, seneta wa Uasin Gishu Margaret Kamar au  Poghisio. Kazi ya Kihika nayo huenda ikapewa   seneta wa wa Murang’a   Irungu Kanga'ta au mwenzake wa  Nairobi Johnson Sakaja.