Usikanyage Kiambu, wabunge wamuonya Ruto

UHURUTO
UHURUTO
Wabunge wanaopinga kampeni za mapema za Naibu Rais William Ruto wanamtaka asikanyage katika kaunti ya Kiambu kama hatakuwa akiandamana na Rais Uhuru Kenyatta.

Wabunge hao wa mrengo wa “kieleweke” pia walimshauri naibu rais kujiuzulu wadhifa huo kama hawezi sitisha kampeni zake za urais mwaka za 2022.

Katika taarifa yenye ujumbe mkali wa kisiasa, wabunge hao walimkashifu Ruto kwa kujipenyeza katika ngome ya rais Uhuru Kenyatta badala ya kumuomba rais baraka zake.

" Hukaribishwi katika kaunti hii kama hutaandamana na Uhuru,” alisema mbunge wa zamani George Nyanja.

Mbunge huyo wa zamanai aliuliza: “Mtu anaweza aje kwenda kwa boma la mwenzake bila mwenyeji kujua?"

Alimkashifu Naibu Rais ambaye amekuwa akizunguka maeneo mbali ya nchi akiongoza mikutano ya kuchangisha pesa kusaidia makanisa na kumtaka aonyesha imani yake kwa Mungu kwa kujenga upya makanisa yote yalioharibiwa wakati wa machafuko ya baada ya uchaguzi mwaka 2007/08.

"Kanisa la Kiambaa liliteketezwa wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi. Watu walifariki ndani ya kanisa hilo huku wengine wakiachwa na makovu maisha yao yote, wacha Ruto ajenge kanisa hilo ikiwa ni kweli amejitolea kujenga makanisa kote nchini," Alisema.

Nyanja aliyasema haya katika eneo la Githunguri.

Kwingineko katika kaunti ya Nairobi baadhi ya wabunge wa Jubilee wakiongozwa na mbunge wa Cherengany Joshua Kutunyi walimtaka Ruto kumheshimu kiongozi wake na manifesto ya chama cha Jubilee.

Anasema hii inajumuisha kuunga mkono kikamilifu agenda kuu ne za serikali ambazo zinalenga kuimarisha maisha ya mamilioni ya wakenya.