Usitie guu mkoa wa Magharibi, wabunge wamwonya Ruto

western-compressed
western-compressed
Wabunge sita kutoka mkoa wa magharibi wamemuonya DP William Ruto kutokanyaga eneo hilo baada ya wakaazi kutoka jamii ya Luhya kufukuzwa kule Nandi.

Wakiongozwa na seneta wa Kakamega Cleophas Malala, sita hao wamesema Ruto hatakaribishwa iwapo wale waliofurushwa makwao hawatarejeshwa katika ardhi yao.

Takriban familia 1,500 zimekosa makaazi baada ya kufurushwa huko Nandi huku ikidaiwa ni mzozo wa ardhi.

Wabunge wanasema nyumba, makanisa na shule zilibomolewa wakati wa uvamizi huo Jumatano usiku.

"Nataka kuliweka jambo hili bayana, nataka kumwambia Naibu Rais kuwa hajakaribishwa katika eneo letu ikiwa watu wetu bado wanafurushwa kutoka Nandi," Malala aliambia waandishi wa habari Alhamisi.

Wabunge wengine waliokuwapo ni; Caleb Amisi wa Saboti, Florence Mutua ambaye ni mwakilishi wa wanamke wa Busia, George Aladwa wa Makadara, mbunge mteuliwa Godfrey Osotsi na katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna.

Osotsi alisema jamii haitakubali jinsi marusho hayo yalivyofanywa kwa njia ya kinyama.

"Hatutaki kuwa na marafiki tu wanapokuja kutafuta kura," Osotsi alisema.

Viongozi hao walimtaka Rais Uhuru Kenyatta aingilie kati wakihofia idadi kubwa ya watahiniwa kukosa mitihani yao ya kitaifa mwaka huu.

Ruto amekuwa akizuru mkoa wa Magharibi mara nyingi na anatarajiwa kuhudhuria mazishi ya mke wa kwanza wa seneta wa zamani wa Kakamega Boni Khalwale huko Ikolomani Jumamosi.