"Uso wangu ulikuwa kama nyama ilioteketezwa," - Kelvin Kairo

Kelvin Kairo mwanaume mtanashati aliyeponea shambulio la asidi kali kutoka mahasidi wake ambayo hadi leo hajawafahamu wala kubaini lengo lao la kumwagikia kemikali hiyo na kuharibu uso wake.

"Baada ya kulazwa kwa majuma mawili, nilijiona kwenye kioo na kile nilichoona sikuamini, uso wangu ulikuwa kama nyama ilioteketezwa"

Kairo ambaye alikuwa ameamua kujiua baada ya mkasa huo, aliponea baada ya sumu yake kupunguzwa makali na tembe alizokuwa akimeza kila siku.

Kwa sasa, Kairo ambaye ndiye mume wa Grace Naito na baba wa watoto wawili anasimulia tukio hilo ambalo ijapokuwa limepona, limebakia kuwa kovu la moyoni kila mara anapojitazama kwa kioo.

‘Nilikuwa nikitembea kuelekea kazini kwangu Machi 2018. Ilikuwa mwendo wa saa 5.30 alfajiri. Laiti ningalijua kwamba kuna jamaa aliyekuwa akinisubiri, nisingalienda kazini siku hiyo.

Nilipokaribia watu waliokuwa wamesimama, walinimwagia likwidi kwenye uso wangu. Sikuwatambua hao walikuwa kina nani, ila nilibahatika kutorokea usalama wangu." Kairo anasimulia masaibu hayo.

Kairo anasema kwamba alihisi baridi kwanza, kisha kukawa na mwasho mkali sana usoni mwake.

"Kwa mshtuko, singejua iwapo mahasidi hao walikuwa wamenifuata ila nilikimbia katika duka kuu lililokuwa karibu na eneo hilo huku nikiomba msaada kutoka askari waliokuwa karibu." Kairo anasema.

"Niliwaambia wanisaidie maji kuosha uso wangu" alisema.

"Walinisaidia kuosha uso wangu lakini nilikuwa nimepofuka. Singeweza hata kuona simu yangu. Askari hao walinisaidi kuwapigia jamaa wangu waliokuja kunipeleka hospitalini"

Anasema kwamba alilazwa hospitalini kwa majuma mawili akiwa kipofu kabla ya kupata uwezo wa kuona tena.

Mke wake alimsaidia sana kwa kuwa alikuwa akimpa dawa kila baada ya dakika 15.

"Kwa wakati moja, hata nilitaka kujiua, sumu niliokunywa uliisha ukali kutokana na dawa nilizokuwa nimemeza muda mfupi"

Kairo ambaye alikuwa ameamua kujiua baada ya mkasa huo, aliponea baada ya sumu yake kupunguzwa makali na tembe alizokuwa akimeza kila siku.

Kwa sasa amekata kauli hiyo ya kujitoa uhai na  anasifia mke wake kwa kumlisha, kumlinda hospitalini na hata kumrai kukubali hali yake jinsi ilivyo.

"Nimeshauriwa kwenye kituo cha ushauri nasaha kubadilisha mawazo yangu na kuwa na mtazamo chanya kuhusu maisha yangu" alisema.