Vichwa Maji! Watu 9 waliohepa Nairobi kupitia njia za mkato wanaswa

Watu tisa waliofaulu kuondoka katika eneo la Nairobi na viunga vyake ambalo limefungwa wamekamatwa katika kaunti ya Murang'a. Wanaume hao watano, wanawake watatu na mtoto mmoja walikamatwa katika kizuizi siku ya Jumatatu, Mei 11, baada ya kushindwa kutoa stakabadhi za kuwaruhusu kusafiri.

Akithibitisha kukamatwa kwao, OCPD wa Murang'a Mashariki, Alex Muasya, alisema washukiwa walikuwa wameabiri matatu kutoka Kenol, kaunti ya Kiambu na kutumia njia za mkato kuingia Kaunti ya Murang'a.

"Wakati waliwasili katika kizuizi, waliulizwa stakabadhi zao za kusafiri na kuibuka hawana."Amesema Alex Muasya

Washukiwa sasa wamepelekwa katika makao makuu ya polisi kaunti ya Murang'a kabla ya kuhamishwa hadi kituo cha karantini huku wakisubiri kupelekwa kortini baada ya siku 14.

Hata hivyo, si mara ya kwanza kwa kisa sawia na hicho kuripotiwa Murang'a, ambayo imeibuka kuongoza katika kukiuka maagizo ya serikali kukabiliana na COVID-19 na pia kutumia mbinu za kiasili kukabili ugonjwa huo.

Mnamo Aprili 15, zaidi ya wafanyakazi 52 ambao walikuwa wanasafari katika lori moja walikamatwa eneo la Maragua wakiwa safarini kuelekea shambani. Walipelekwa katika kituo cha polisi cha Maragua kabla ya kuhamishwa hadi katika Shule ya Wavulana ya Chania ambapo waliwekwa karantini kwa siku 14.