Viongozi wa kidini waunga mkono wito wa Rais kukabili ukeketaji wa wanawake

Wazee wa jamii na viongozi wa kidini kutoka kote nchini hii leo waliazimia kumaliza ukeketaji wa wanawake nchini itimiapo mwaka 2022.

Viongozi hao walifanya azimio hilo katika Ikulu ya Nairobi wakati wa mkutano na Rais Uhuru Kenyatta na Mama wa Taifa Margaret Kenyatta.

Azimio hilo la viongozi kutoka kaunti 22 ambako ukeketaji wa wanawake hufanyika kwa wingi linaunga mkoo tangazo la Rais Kenyatta la kumaliza utamaduni huo wa kihalifu nchini itimiapo mwaka 2022.

“Tunatambua juhudi za serikali za kumaliza Ukeketaji wa Wanawake kupitia ubunifu na utekelezaji wa sera zenye manufaa, mikakati ya kisheria na mipango ya kuukabili,” kasema Josephat Murangiri, ambaye ni Katibu Mkuu wa baraza kuu simamizi la wazee wa Meru (Njuri Ncheke) ambaye alisoma azimio hilo la wazee.

Kama sehemu ya juhudi zao za kukabiliana na ukeketaji wa wanawake,  viongozi hao walijitolea kushirikiana na kufanya kazi na serikali ya kitaifa na zile za kaunti pamoja na washika dau wengine kutoa uhamasisho kwa jamii kuhusu haja ya kuendeleza elimu na hali bora ya mtoto msichana.

Akizungumza kwenye sherehe hiyo ambayo pia ilitumiwa kuzindua sera ya kitaifa ya kukabiliana na Ukeketaji wa Wanawake, Rais Kenyatta aliwapongeza wazee hao na viongozi wa kidini kwa kuafikiana kukabili mila hiyo potovu na akawahakikishia serikali itawaunga mkono.

Rais alisema Ukeketaji wa Wanawake ni mila iliyopitwa na wakati ambayo inaathiri ufahamu wetu binafsi na kitaifa na akapigia debe juhudi za kuukabili kabisa.

“Ukeketaji wa Wanawake ambao umekuwepo nchini ni mila potovu ambayo hakika inahujumu ufahamu na hadhi yetu kibinafsi na pia kitaifa.

"Utamaduni huo ni kikwazo kwa maadili yetu ya pamoja ilivyo kwenye katiba yetu ambayo tuliipitisha kama Wakenya,” kasema Rais.

Alitoa wito kwa Wakenya kujiepusha na mila potovu kama vile Ukeketaji wa Wanawake na watilie maanani shughuli za kitamaduni zenye maendeleo zinazowapa wanawake na wasichana heshima na hadhi.

“Kama ilivyo katika mambo yote, wakati hufika ambapo mtu hukumbana na njia mpya za maisha.  Sasa ni wakati wetu sote kuacha mila potovu kwa ajili ya taifa,” kasema Kiongozi wa Taifa.

Rais aliagiza maafisa wa serikali katika wizara husika za Jinsia, Elimu, Afya na Utawala wa Umma kuongoza juhudi za serikali za kukomesha ukeketaji wa wanawake kote nchini.

“Ukipata afisa wa serikali yeyote awe chifu au naibu wake anayeunga mkono mila hii potovu, piga ripoti kwa afisi zinazofaa na atachukuliwa hatua kali,” Rais alionya.

Rais alitaharisha jamii zinazoishi mipakani na wanaotorokea nchi jirani kuwakeketa wanawake akisema anashauriana na marais wenzake kuhakikisha wanaotekeleza uhalifu huo wanaadhibiwa katika nchi hizo.

Mwakilishi wa shirika la UNFPA hapa nchini Dkt. Ademola Olajide aliyehutubia hafla hiyo alisema ukeketaji wa wanawake ni mojawapo wa ukiukaji wa haki wa mapema kwa wanawake na wasichana.

Alisema upashaji tohara una madhara makubwa ya kiuchumi na kiafya kwa wanaoathiriwa.

Dkt Olajide alimshukuru Rais Kenyatta na Mama wa Taifa Margaret Kenyatta kwa kuongoza vita dhidi ya ukeketaji wa wanawake na akawahakikishia kwamba shirika lake litawaunga mkono kikamilifu kuhakikisha nchi hii inakomesha uovu huo kufikia mwaka wa 2022.

Kwa upande wake, Waziri wa Jinsia Margaret Kobia alimpongeza Mama wa Taifa kwa mchango wake mkubwa kukuza afya ya akina mama wanaojifungua na watoto wachanga , na kuwalinda wanawake kupitia kwa shirika la Beyond Zero kutokana na madhara ya ukeketaji kama vile ugonjwa wa kuvuja mkojo.

Rais na Mama wa Taifa Margaret Kenyatta walitunukiwa bangili za ushanga kuwaheshimu kutokana na juhudi zao katika kupambana na ukeketaji wa wanawake.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia Joseph Mucheru, Balozi wa Canada hapa nchini Lisa Stadelbauer na Balozi wa Autria Dkt Christian Fellner pia walihudhuria hafla hiyo iliyohutubiwa pia na Katibu Msimamizi Rachael Shebesh.

 -PSCU