Viongozi wa Tharaka nithi wapinga matokeo ya sensa

njuki
njuki
Viongozi kutoka kaunti ya Tharaka Nithi wametishia kuchukua hatua ya kuenda kortini kupinga matokeo ya sensa ya mwaka huu.

Wakiongozwa na Gavana Muthomi Njuki, viongozi wa kaunti hiyo walisema kuwa matokeo hayo hayaonyeshi ni nini nchi hii halitambui kuhusu kaunti hiyo.

Kulingana na ripoti ya sensa ya 2019 iliyotolewa siku ya jumatatu, kaunti hiyo ya Tharaka Nithi ilikuwa na watu 393,177 waliosajiliwa ikilinganishwa na ripoti ya sensa ya mwaka 2009 ambayo ilionyesha kuwa kaunti hiyo ilikuwa na watu 365,330.

 Kaunti hiyo ilitambulika sana kwa kuwa na wapiga kura wengi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Gavana Njuki alisema kuwa matokeo ya idadi ya watu ni muhimu kwani yanaonyesha rasilimali ambayo kaunti hiyo itapokea.

Wanasema kuwa matokeo ya sensa ni dhulma kwa kaunti hiyo.

Mbunge wa Maara Kareke Mbiuki alisema kuwa matokeo hayo ya sensa hayaonyeshi idadi ya kaunti hiyo.

Walieleza kwamba ripoti ya hapo awali ilikadiria idadi ya watu wa kaunti hiyo kuwa  480,000.

Viongozi hao walisema kuwa ripoti hiyo isipokaguliwa, basi wataenda mahakamani kuhakikisha kuwa ripoti ya sensa ya kaunti hiyo imefutiliwa mbali.

Viongozi hao pia walitaka KNBS kutoa ufafanuzi kuhusiana na wakazi wa Tharaka Nithi waliohesabiwa nje ya kaunti hiyo.