Stori za Ghost: Jamaa adai fidia ya nusu milioni baada ya kufumania mkewe akijamiiana na bwenyenye kwake nyumbani

Muhtasari

•Dereva yule aliondoka pale nyumbani na akaenda kupolea mahali akisuburi wakati mwafaka wa kufumania mkewe akiwa kwenye kitendo.

•Kwa wakati huo mwenye nyumba alikuwa amejihami kwa kisu na upanga tayari kuchukua sheria mkononi dhidi ya fisi aliyekuwa ananyemelea mkewe.

•Jamaa aliridhika na fidia ambayo alipata kutoka kwa bwenyenye huyo na akamuachia mkewe waendeleze mahusiano yao.

Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha 'Stori za Ghost', mtangazaji Ghost Mulee alisimulia kisa kimoja ambapo jamaa mmoja anasemekana kulazimika kulipa fidia ya nusu milioni baada ya kufumaniwa na mke wa wenyewe.

Kulingana na Ghost, jamaa huyo amekuwa akijiburudisha na mke wa dereva wa trela kwa kipindi kirefu ila siku zake arubaini zilikuwa zimetamatika.

"Mwenye nyumba ni jamaa wa trela, ni dereva  wa masafa marefu. Alikuwa ameshadokezewa kwamba kuna jamaa huja pale nyumbani kwake anapoondoka. Akaambia mkewe kwamba anaenda Kigali kwa ziara ya siku kama nane" Ghost alisimulia.

Dereva yule aliondoka pale nyumbani na akaenda kupolea mahali akisuburi wakati mwafaka wa kufumania mkewe akiwa kwenye kitendo.

Baada ya kuwa mbali na kwake kwa siku nne, dereva huyo alipigiwa simu na jirani na kuarifiwa kwamba mkewe alikuwa ameleta jamaa pale nyumbani.

"Jamaa alipokuja na kubisha mlango bibi akamuuliza 'ni nani huyo?' Jamaa akasema 'ni bwanako, mimi ni mwenye nyumba' Bibi akamwambia kuwa bwanake alienda Kigali" Ghost alisimulia.

Kizaaza kikubwa kikatokea pale huku halaiki ya watu ikijumuika kushuhudia drama ile. Kwa wakati huo mwenye nyumba alikuwa amejihami kwa kisu na upanga tayari kuchukua sheria mkononi dhidi ya fisi aliyekuwa ananyemelea mkewe.

"Mzee alisema bila nusu milioni hatang'atuka pale. Ilibidi jamaa aliyekuwa ndani atoe nusu milioni. Mwenye nyumba alipatiwa pesa zake akasema wameachana na mkewe" Alisimulia Ghost.

Jamaa aliridhika na fidia ambayo alipata kutoka kwa bwenyenye huyo na akamuachia mkewe waendeleze mahusiano yao.