Waganga wa Kitui wasema walisaidia kukamatwa kwa washukiwa waliotoroka Kamiti, wadai 10% ya Sh60M zilizoahidiwa

Muhtasari

•Waganga hao wanadai uganga wao ulisaidia katika kukamatwa tena kwa Musharraf Abdalla, Joseph Juma na Mohammed Abdi ambao walikamatwa katika eneo la Mwingi siku tatu baada ya kufanikiwa kutoroka.

Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha 'Story za Ghost', mtangazaji Ghost Mulee alizungumza kuhusu madai ya waganga kutoka kaunti ya Kitui.

Kulingana na Ghost, Waganga wa Kitui sasa wanadai kugawiwa asilimia kumi ya shilingi milioni 60 ambazo serikali iliahidi kuzawadi yeyote ambao angesaidia kukamatwa tena kwa washukiwa wa kigaidi ambao walitoroka kutoka jela ya Kamiti mnamo Novemba 15.

Waganga hao wanadai uganga wao ulisaidia katika kukamatwa tena kwa Musharraf Abdalla, Joseph Juma na Mohammed Abdi ambao walikamatwa katika eneo la Mwingi siku tatu baada ya kufanikiwa kutoroka.

"Waganga wa Kitui sasa wamekutana na kudai wanataka asilimia kumi ya pesa hizo kwa sababu waasema wao ndio walitumia uganga wao wale magaidi wakashindwa kuvuka Kitui. Wanasema walipopata zile habari walipiga ramli alafu wale magaidi wakachanganyikiwa wakashikwa . Sasa wanaomba angalau mgao wa asilimia kumi ya zile pesa" Ghost alisema.

Alisema waganga hao hawataki kuulizwa maswali mengi kuhusiana na tukio hilo huku wakitishia kutenda uganga mwingine.

Serikali ilikuwa imeahidi zawadi ya milioni 60 kwa yeyote ambaye angetoa taarifa ambazo zingesaidia kukamatwa kwa washukiwa hao watatu wa kigaidi.

Watatu hao walikamatwa tena mnamo Novemba 18 huku watu mbalimbali wakijitokeza kudai walifanikisha kukamatwa kwao.

Serikali ilitoa hakikisho kwamba watu ambao kwa  kweli walisaidia wangepokea zawadi yao kama ilivyoahidiwa.

Hata hivyo serikali iliapa kutofichua atakayepokea kwa sababu za kiusalama kwani washukiwa wale walikuwa wamefungwa kufuatia madai yenye uzito.