Mtangazaji Gidi asherehekea baada ya kuhitimu kama Mwanasayansi wa Data

Mtangazaji huyo alihitimu baada ya kukamilisha masomo katika Shule ya Biashara ya McCombs.

Muhtasari

•Gidi alihitimu na kupokea cheti chake kutoka Chuo Kikuu cha Texas baada ya kumaliza masomo yake ya Uzamili katika Sayansi ya Data na Uchambuzi wa Biashara.

•Mtangazaji mwenzake, Jacob 'Ghost' Mulee alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kumpongeza kwa ushindi huo.

Image: GIDI OGIDI

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Joseph Ogidi Oyoo almaarufu Gidi sasa ni mwanasayansi wa data aliyeidhinishwa.

Gidi alihitimu na kupokea cheti chake kutoka Chuo Kikuu cha Texas katika jimbo la Austin, Marekani baada ya kumaliza masomo yake ya Uzamili katika Sayansi ya Data na Uchambuzi wa Biashara katika Shule ya Biashara ya McCombs.

Huku akisherehekea ushindi huyo, mwimbaji huyo wa zamani alitoa shukrani za dhati kwa chuo hicho cha Marekani kwa mafunzo aliyopokea.

"Mwanasayansi wa Data aliyeidhinishwa, asante Chuo Kikuu cha Texas, Shule ya Biashara ya McCombs kwa mafunzo ya kina," alisema.

Mtangazaji huyo aliambatanisha ujumbe wake na picha ya cheti ambacho alikabidhiwa baada ya kukamilisha masomo yake.

Cheti hicho kilionyesha kuwa alihitimu mwezi uliopita, Machi.

Mtangazaji mwenzake, Jacob 'Ghost' Mulee alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kumpongeza kwa ushindi huo.

"Hongera bosi," alisema.

Gidi alijiunga na shule ya upili ya Aquinas kisha kuendeleza masomo yake katika vyuo vikuu vya JKUAT na KCA.

Mwezi uliopita, mtangazaji huyo alianza jaribio lake la nne la kujifunza lugha ya Kifaransa baada ya kushindwa katika majaribio yake matatu ya awali.

Katika tangazo lake, mtangazaji huyo mahiri alieleza matumaini yake kuwa mara hii hatimaye atafanikiwa kusoma lugha hiyo ya kigeni.

"Hili litakuwa jaribio langu la 4 lakini safari hii nina matumaini kuwa nitafanikiwa," alisema kwenye mtandao wa Instagram.

Mtangazaji huyo alifichua kuwa safari yake ya nne ya kujifunza Kifaransa ilianza baada ya kuchapisha video ya binti yake, Marie-Rose, akijaribu kumfundisha lugha hiyo takriban  miezi miwili iliyopita.

"Watu wengi walionitakia heri nchini Ufaransa na Kenya walijitolea kunisaidia kujifunza Kifaransa. Hatimaye nilifuatiliwa kupitia Ubalozi wa Ufaransa na Alliance Francaise ambao wametoa mpango wa ushirikiano kujifunza Kifaransa," alisema.

Katika video iliyochapishwa mwezi Januari, Marie-Rose alionekana akimfundisha baba yake maneno ya Kifaransa. Rose alicheka sana lafudhi ya baba yake alipokuwa akijaribu kurudia maneno ya Kifaransa baada yake.