Katika kitengo cha Patanisho, dereva aliyejitambulisha kama Felix Omondi ,31, kutoka Homa Bay alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Evelyn Atieno ,26, ambaye alikosana naye mwezi mmoja uliopita.
Felix alisema ndoa yake ya miaka sita iliingia doa wakati alipoamua kumpima mkewe iwapo anaweza kubali kuwa na mke mwenza.
"Nilimuoa mke wangu nikiwa katika chuo kikuu, alikuwa na miaka 20. Baba yangu alikuwa na wake wengi. Ata mimi nilitaka niwe na familia kubwa. Nilitaka niwe na bibi wawili, ama watatu. Wakati nilimuoa, nilikuwa nimemwambia kwamba nitaongeza bibi," Felix alisema.
Aliongeza, "Hivi majuzi kuna mwanamke nilipata. Bibi yangu hajawahi taka mambo ya kuletewa bibi mwingine, anataka awe peke yake. Nilimweleza huyo mwanamke kila kitu, nilitaka tu kujua kitu kama hilo likitokea, itakuwaje."
"Kuna siku nilikuwa nachat na huyo mwanamke, bibi yangu akapata hizo meseji. Nilimwambia huyo ni ex wangu ambaye amerudi na nataka awe bibi wa pili. Bibi yangu alichukua namba wakawa wanaongea."
Felix alisema mambo yalibadilika kabisa nyumbani wakati mkewe alipopata jumbe zake na mwanadada huyo akimwambia anataka kumuoa. Alisema jambo hilo lilimuathiri sana mkewe kiasi cha kushindwa kudhibiti hisia.
"Mwezi mmoja uliopita, bibi yangu alipata meseji nikimwambia huyo msichana kwamba nataka nimuoe kama mke wa pili. Toka apate hizo meseji, mke wangu analia tu kwa nyumba. Hata akipika analia tu. Bibi yangu ni yatima, hana baba hana mama. Kila saa anaangalia picha za mama yake akilia. Naona kama mke wangu anapagawa. Hata nimebadili msimamo wangu sitaki mke wa pili. Nampenda mke wangu sana," alisema.
Kuhusu mwanamke ambaye alikuwa akiongea naye, Felix alisema, "Huyo hatuongei. Hiyo stori nilikata kabisa. Nilimwambia hiyo stori iishe kabisa. Kama hiyo kitu ambayo si ya kweli ako karibu kuchizi."
Evelyn alipopigiwa simu alidhibitisha madai ya mumewe.
Hata hivyo aliweka wazi kwamba tayari wamezungumzia suala hilo na amemsamehe Felix.
"Kulingana na ushahidi ambao nilipata, nilidhani ni ukweli lakini alishaniongelesha. Kwa sasa sina shida na yeye," alisema.
Felix alimwambia, "Ile mood ambayo uko nayo kwa nyumba, sipendi hivyo. Hiyo nia ya kuongeza bibi sina kabisa. Nataka tuishi na wewe tulee watoto wetu. Kama itawezekana tuishi milele na milele bila kufa. Kama kuongeza bibi ndiyo itaharibu ndoa yangu, wacha ikae."
"Mpenzi mimi nakupenda sana. Kwanzia leo hakuna kitu utaniambia nikose kuskia. Nakupenda nataka tuishi na amani maisha yetu yote."
Evelyn alisema, "Nilimsamehe kitambo sana. Akirudia tena kitamramba."
Huku akimjibu, Felix alisema, "Mimi sitawahi kurudia. Nimeona na macho yangu, bibi yangu karibu akufe. Mbele ya mwenyezi Mungu, sijawahi kuwa na mpango wa kando. Huyo mwanadada hata sikuwa nimelala naye, ni ile kumleta karibu na mazungumzo."
Felix ambaye alisikika kujazwa bashasha na jambo hilo aliahidi kumpeleka mkewe likizoni Mombasa na hata kufichua kuwa tayari amekata tiketi.
"Nitakupeleka Mombasa. Tuende tujivinjari utoe stress na tuendelee na maisha. Tiketi nilishakata ya Jambo Jet, acha nipeleka bibi kwa beach. Huyo mama ni malaika, sitaki mtu acheze na yeye," Felix alisema.
Evelyn alimwambia, "Afanye jambo sawa. Mapenzi anajua iko. Asinisukume kwenye ukuta."