Siku ya Jumatano asubuhi, jamaa aliyejitambulisha kama Julius Munguwe ,31, kutoka Tanzania alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Jane Kemuma Nyabuto ,24, ambaye alikosana naye mwezi uliopita.
Julius alisema ndoa yake ya miaka sita ilisambaratika takriban wiki mbili zilizopita kufuatia mizozo ya kinyumbani.
"Nilikosana Na mke wangu kuanzia mwezi wa pili. Tumekuwa tukizozana kwa muda lakini mnamo Februarii 28, kuna simu ambayo alipigiwa iliyofanya nireact. Baada ya kupigiwa simu niliamua kuchukua hatua ambayo ilikuwa mbaya,” Julius alisimulia.
Aliendelea, “Tayari alikuwa ameshajipanga ataondoka. Alikuwa ameongea na jamaa wa mpesa kwa sababu alitaka tukiachana, aanze hiyo biashara. Jamaa huyo hata hivyo hakuenda direct kumwambia ameshughulikia suala lao. Jamaa alimuuliza umekula nini?, nilishangaa kwa sababu hajawahi kupigiwa simu kama hiyo usiku tena nikaamua kureact kwa hasira.”
Julius alisema mkewe alichanganya suala hilo na mambo mengine ambayo wamezozania katika siku za nyuma kisha akaondoka.
Aidha, alifichua kuwa walikuwa wakizozana kuhusiana na mambo ya kibiashara ambapo alikuwa akichukua mali yake bila kulipa.
Jane alipopigiwa simu aliweka wazi kwamba ni ngumu kwake kukubali ombi la baba huyo wa mtoto wake mmoja kwa sasa kwani alimkosea sana.
Pia alifichua kwamba mume huyo wake alikuwa akimtegemea kwa kila kitu nyumbani.
“Huyo jamaa hakuna kitu alikuwa ananisaidia kwa nyumba. Ni kama nilikuwa nimemuoa. Nilikuwa nalipa nyumba, nanunua chakula, nashughulikia mtoto. Ukiona nimeondoka nikaenda kuishi kando nimechoka kabisa,” alisema.
Pia alifunguka kuhusu baadhi ya nyakati ambapo Julius alimkosea ikiwemo kipindi alitaka kumchoma yeye na mtoto ndani ya nyumba.
“Sitalisha mtoto na nilishe mtu mzima,” alisema
Julius aliomba msamaha na kujitetea akisema, “Nilipata ajali wakati huyo mama alikuwa na mimba ya mtoto ambaye analea. Kitu ambacho kilileta shida ni ule mkopo nilikuwa nashughulikia.”
Jane hata hivyo alibainisha kwamba anahitaji muda wa kufikiria kabla ya kuamua kama atarudi.
“Nahitaji muda nijui nilikosea wapi. Anipee muda kidogo mimi mwenyewe nitamtafuta. Anipee kama mwezi hivi,” alisema Jane.
Julius alisema, “Naomba asiniwekee sana. Asiniblock. Anipee uwezo wa kumpigia simu nikimhitaji.”
Pia alikiri kuwa Jane amekuwa nguzo muhimu katika maisha yake na akamuomba arudi.
Je, maoni yako kuhusu Patanisho ya leo ni yepi?