Mwanaharakati kijana, Samuel Makori almaarufu Kasmuel McOure, amekanusha madai kwamba alifukuzwa kutoka Shule ya Upili ya Wavulana ya Alliance.
Katika mahojiano na Radio Jambo Digital mnamo Alhamisi asubuhi, msanii huyo mwenye umri wa miaka 26 hata hivyo alikiri kuwa mtukutu baada ya kuingia kidato cha 2 katika Alliance.
Alifichua kuwa alisimamishwa kutoka shule mara kadhaa kabla ya kuondoka kabisa katika shule hiyo ya upili iliyoko Kiambu hadi shule nyingine ya upili ya kitaifa ya Maranda.
“Nilianza kuwa mtukutu nikiwa kidato cha pili kama kijana mwingine yeyote. Haikuwa 4G, ilikuwa ni kusimamishwa. 4G ni kama kitu cha kujitolea. Nilibadilisha shule kwa sababu ya maisha, kuna maisha katika shule ya upili, kuna kuchunguza, sijui nini. Ni maisha tu,” Kasmuel alisema.
Kijana huyo ambaye amehusika sana katika maandamano ya hivi majuzi dhidi ya serikali alifichua kuwa alisimamishwa shule mara kadhaa katika siku zake za shule ya upili.
Pia alizungumza kuhusu maisha yake ya uhusiano akifichua kuwa kwa sasa anachumbiana.
"Ndiyo, nina uchumba," alisema.
Aliongeza, "Kuchumbiana ni kitu kizuri, ningekushauri uifanye. Kuwa na mtu unayempenda, mtu unayemheshimu, mtu ambaye ni rafiki yako. Nadhani hiyo ni nzuri sana."
Akizungumzia siasa za vijana, alizungumza dhidi ya kuundwa kwa chama cha Gen-z akisema kitakuwa cha kibaguzi kwani kitawakilisha kikundi cha rika fulani tu.
"Tafuta chama ambacho kinakufanyia kazi, chama ambacho unaheshimu maadili, misimamo na harakati zake na ujiunge nacho," alisema.
Kasmuel amekuwa akivuma sana kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa mengine ya vyombo vya habari katika wiki za hivi majuzi kutokana na kuhusika kwake sana katika maandamano ya kuipinga serikali.