"Baby Pendo sasa amepumzika" Gidi azungumza baada ya mpwa wake mdogo kuzikwa

Pendo alizikwa nyumbani kwa babu yake, katika kijiji cha Okok, eneo la Ndiwa, Kaunti ya Homa Bay.

Muhtasari

•Gidi alichapisha picha na video kadhaa za hafla hiyo iliyojaa hisia kali kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

•Hali ya huzuni ilitanda hewani wakati malkia huyo mdogo akizikwa.

Mpwawake gidi, Pendo
Image: INSTAGRAM// GIDI OGIDI

Mpwa mdogo wa mtangazaji Gidi, Laviliah Lippens almaarufu Baby Pendo hatimaye alizikwa siku ya Jumatatu.

Pendo ambaye alikuwa binti pekee wa dada mdogo wa Gidi alizikwa nyumbani kwa babu yake, katika kijiji cha Okok, eneo la Ndiwa, Kaunti ya Homa Bay. 

Gidi alichapisha picha na video kadhaa za hafla hiyo iliyojaa hisia kali kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Imekuwa wiki yenye shughuli nyingi lakini Baby Pendo sasa amepumzika,” alisema chini ya picha alizochapisha.

Mwili wa Pendo ambao uliwekwa kwenye jeneza jeupe ulibebwa na waliokuwa wenzake katika brigedi wa kanisa la SDA.

Hali ya huzuni ilitanda hewani wakati malkia huyo mdogo akizikwa.

Pendo alikuwa na umri wa miaka saba tu alipokumbana na kifo chake cha ghafla siku ya Jumapili, Januari 15.

Mpwa huyo wa Gidi aliugua alipokuwa kwenye kambi ya kujivinjari katika kaunti ya Machakos mnamo Januari 11 na akapelekwa hospitalini ambako alitibiwa na kuruhusiwa baada ya kupewa dawa kadhaa.

Hata hivyo,takriban siku nne baadaye, Januari 15, alipelekwa katika hospitali ambako aliaga mwendo wa mbili jioni.

Hapo awali Gidi alifichua kwamba siku moja kabla ya kukutana na kifo chake, marehemu Princess Pendo alikuwa amehudhuria ibada ya kanisa na hata alikariri mstari wa Biblia mbele ya waumini.

"Huyu ni mpwa wetu Princess Pendo akikariri mstari wa Biblia Jumamosi iliyopita katika kanisa. Aliaga dunia siku iliyofuata (Sunday iliyopita)😥😥😥," aliandika chini ya video ya msichana huyo mdogo akikariri mstari wa Biblia.

Katika video ambayo mtangazaji huyo mahiri alichapisha, marehemu Pendo anasikika akikariri mstari wa Biblia kutoka Zaburi 23:6. 

"Hakika wema na fadhili zitanifuata siku zote za maisha yangu, nami nitakaa nyumbani mwa BWANA milele," alikariri kwa Kiingereza.

Gidi alitangaza habari za kifo cha mpwa huyo wake siku ya Jumatatu asubuhi kupitia ukurasa wake wa Instagram.

"Tulikuwa na usiku mrefu lakini wacha nishukuru hospitali, jirani yangu Wakili na marafiki ambao walituunga mkono katika mchakato wa kuhamisha mwili wake hadi chumba cha kuhifadhi maiti," aliandika.

Roho ya Baby Pendo ipumzike kwa amani.