Sitamhukumu Bahati anajua kwa nini anafanya anavyofanya-Benachi

Muhtasari
  • Msanii Benachi asema Bahati amekuwa na bidii sana katika kazi yake
  • Benachi alifahamika sana baada ya kutoa kibao akimshirikisha mwendazake Kaberere
Msanii Benachi
Image: Studio

Katika kitengo cha ilikuaje tulikuwa naye msanii wa nyimbo za injili Benachi, ambaye amekuwa Marekani kwa miaka sita.

Benachi alifahamika sana baada ya kutoa kibao akimshirikisha marehemu Kaberere.

Mwanamuziki huyo amesema kwamba, ni mfanyibiashara na zaidi ya yote anapenda kuimba na kumtukuza Mungu.

"Nimekaa Marekani kwa miaka 6 sasa. Nina watoto 2... Mimi napenda muziki sana. Sijifanyii, nafanyia Mungu. Siwezi kupoteza matumaini. Ilinichukua muda sana kuelewa ni kwa nini nafanya muziki.

Nimezaliwa na kulelewa Kenya ila sasa hivi naishi Atlanta Georgia. Mimi ni mfanyibiashara... napenda Marekani kwa sababu wanapenda watu.

Nimekuja nchini kutembelea familia yangu, na kufanya kazi, nimefanya collabo na Guardian Angel kibao ambacho kitakuwa kwenye Youtube hapo kesho," Alisema Benachi.

Huku akizungumzia suala la msanii Bahati kugura nyimbo za injili alikuwa na haya ya kusema.

"Siwezi kumhukumu Bahati manake anajua ni kwa nini anafanya anavyofanya. Anayajua yaliyo moyoni mwake.

Mtu akiamu kufanya kitu huwa ameamua kwa muda mrefu na huwa na sababu yake ya kufanya hayo.

Bahati amekuwa ndugu na rafiki yangu tumetoana mbali, kile nampendea Bahati sana ni kuwa ni msanii ambaye ana bidii ya kipekee, anatia bidii kwa kazi yake

Kuna pengo katika tasnia ya burudani ya nyimbo za injili kwa maana sio rahisi hivi mwanamuziki kuacha injili,"

Benachi pia alifichua kwamba walitoa kibao na Kaberere wiki mbili kabla ya kifo chake.Kibao hicho kinafahamika kama 'Mwanake'.