"Walikuwa kama rafiki, mume kwangu" Bi Wanjiru azungumzia uhusiano mkubwa kati yake na wanawe waliouawa Kitengela

Wanjiru alisema kuwa alipoenda kutazama miili ya wanawe katika chumba cha kuhifadhi maiti cha KU alishiriki mazungumzo ya mwisho na marehemu mmoja baada ya mwingine.

Muhtasari

•Wanjiru alieleza kuwa mara ya mwisho kuonana na wanawe uso kwa uso wakiwa hai  ilikuwa mwaka wa 2018 alipofunga safari kuenda Uingereza ili kuwatafutia maisha mema.

•Mama huyo alisema kuwa kulikuwa na upendo mwingi kati yake na wanawe kuona kuwa aliwalea peke yake baada ya kutengana na baba yao zaidi ya miaka ishirini iliyopita.

Bi Lucy Wanjiru aliyepoteza wanawe wawili Kitengela
Bi Lucy Wanjiru aliyepoteza wanawe wawili Kitengela
Image: RADIO JAMBO

Mama ya ndugu wawili miongoni wa vijana wanne waliouawa maeneo ya Kitengela Bi Lucy Wanjiru amefunguka kuhusu uhusiano wa karibu uliokuwa kati yake na wanawe. 

Akiwa kwenye mahojiano na Massawe Japanni katika kipindi cha Bustani la Massawe kitengo cha 'Ilikuaje' siku ya Jumanne, Wanjiru ambaye amekuwa akiishi Uingereza kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita alisema kuwa alikuwa akiwasiliana na wanawe Fredrick Muriithi (30) na Victor Mwangi (25) kila siku kabla ya kukumbana na kifo chao.

Wanjiru alieleza kuwa mara ya mwisho kuonana na wanawe uso kwa uso wakiwa hai  ilikuwa mwaka wa 2018 alipofunga safari kuenda Uingereza ili kuwatafutia maisha mema.

"Tulionana  nao mara ya mwisho mwaka wa 2018. Hata hivyo tumekuwa tukiwasiliana nao kila siku" Wanjiru aliambia Massawe.

Mama huyo alisema kuwa kulikuwa na upendo mwingi kati yake na wanawe kuona kuwa aliwalea peke yake baada ya kutengana na baba yao zaidi ya miaka ishirini iliyopita.

Alisema kuwa licha ya kuishi mbali sana na wao alikuwa anashauriana nao mara kwa mara kuhusu masuala mbalimbali ya kimaisha.

"Walikuwa watu wakubwa. Hao watoto wangu walikuwa kama rafiki yangu, mume wangu na mwanangu kwa sababu niliwalea pekee yangu. Tulikuwa na uhusiano wa karibu na tulikuwa tunajadiliana mara kwa mara.. ni watoto wangu wa pekee.. Baba yao alikuwa tu kwa wakati mfupi wakiwa wadogo alafu tukaachana" Alisema Wanjiru.

Wanjiru alisema kuwa alipoenda kutazama miili ya wanawe katika chumba cha kuhifadhi maiti cha KU alishiriki mazungumzo ya mwisho na marehemu mmoja baada ya mwingine.

Alisema kuwa mwanzoni hakuwa ameamini kuwa kwa kweli wanawe wa pekee walikuwa wameaga na alithibitisha kuwa ni kweli wakati aliona mili yao.

"Ilikuwa wakati mgumu kwangu. Vile nilienda kuona kuwa kweli ni wao  walitolewa na nikahakikisha kweli ni wao. Naona watoto wangu walipata kifo cha uchungu sana sababu walikuwa wamedungwa kila mahali. Niliweza kuongea na wao. Watu waliniambia vile nilikuwa naongea. Niliongea nao mtoto mmoja baada ya mwingine lakini baada ya hapo sikujiskia tena nikajipata hospitalini KU nikipokea matibabu"  Bi Wanjiru alisema.

Wanjiru alisema kuwa amekabiliwa na majonzi mazito sana kufuatia kuaga kwa wanawe na hawezi taka mwingine apitie wakati kama ule. 

Alisema kuwa mara kwa mara anajipata akilia kwa nguvu na kupiga nduru usiku haswa anapowaza kuhusu walichokipitia wanawe mikononi mwa wauaji.

"Kuna kitu inanipata usiku nikifikiria vile wanangu walihisi uchungu mwingi walipokuwa wanauawa, walivyolilia huruma. Nafikiria vile watoto walipigwa wakiona wanauliwa. Jana hata nilipiga nduru usiku" Wanjiru alisema.

Amesema kuwa anaomba haki itendeke kwani hivyo tu ndivyo ataweza kupata utulivu wa moyo.