Terence Creative alilia baada ya kufanikiwa kuweka milioni yake ya kwanza kwa simu

Muhtasari

•Amesema kwamba alianza alipojitosa kwenye usanii alianza kuweka pesa kidogo kidogo alizokuwa analipwa baada ya kutumbuiza watu hadi wakati mmoja alipoangalia akagundua kuwa tayari alikuwa amewekeza zaidi ya milioni.

•Amefichua kwamba aliifanya kanuni yake kuweka angalau 30% ya pesa zozote anazopokea ili kuhakikisha kuwa amesalia imara kiuchumi.

Terence Creative katika studio za Radio Jambo siku ya Ijumaa
Terence Creative katika studio za Radio Jambo siku ya Ijumaa
Image: RADIO JAMBO

Mgeni wetu katika kipindi chetu cha Bustani la Massawe kitengo cha 'Ilikuaje?' siku ya Ijumaa alikuwa mwigizaji na mchekeshaji Lawrence Macharia almaarufu kama Terence Creative.

Terence amesema kwamba anafurahia zote anazofanya  huku akikiri wazi kuwa kwa kweli sanaa inalipa.

Amesema kwamba alianza alipojitosa kwenye usanii alianza kuweka pesa kidogo kidogo alizokuwa analipwa baada ya kutumbuiza watu hadi wakati mmoja alipoangalia akagundua kuwa tayari alikuwa amewekeza zaidi ya milioni.

"Sikupata Millioni yangu ya kwanza mara moja. Ilikuwa kuchanga. Nilikuwa napata kidogo kidogo naweka alafu siku moja nikaenda kuangalia nikapata niko na milioni 1.2. Niliwekeza kwa simu" Alisema Terence.

Terence ambaye kwa sasa Wakenya wamembatiza jina 'Ngamwaya' kutokana na filamu yake 'Wash Wash' amesema kwamba aliwekeza akiwa na lengo la kujengea wazazi wake nyumba na kukuza taaluma yake ya usanii.

Amekiri kwamba aliwezwa na hisia na hata kulia baada ya kuona fedha alizokuwa amefanikiwa kuwekeza. 

Amefichua kwamba aliifanya kanuni yake kuweka angalau 30% ya pesa zozote anazopokea ili kuhakikisha kuwa amesalia imara kiuchumi.

Terence ameshauri wasanii wote wasitumie fedha zao zote kujiburudisha ila wazingatie kuwekeza na kugharamia mahitaji ya msingi  ili wasije wakalia baadae.

Hata hivyo amesihi Wakenya kukubali kusaidia wasanii wetu huku akidai kwamba kuna baadhi yao ambao wanapitia wakati mgumu. 

"Tusaidiane kama Wakenya. Kuna wasanii ambao wanaumia. Msanii akikuomba kitu kuna sababu yake msaidie. Kuna wasanii ambao wamelala njaa huku nje, kunao ambao wamefungiwa manyumba lakini wanaogopa kusema wakihofia kuchekwa. Wasanii wanakufa kwa sababu ya msongo wa mawazo" Terence alisema.