Jacky Vike azungumzia vile kuzaliwa kwa mwanawe kuliathiri ndoto yake ya kupata watoto 6

Muhtasari

•Jacky alisema kuwa ana mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka minne ambaye kwa sasa amejikita katika kumpa malezi bora zaidi.

•Alifichua kuwa ndoto yake ilikuwa kupata angalau watoto sita, wazo ambalo lilibadilika baada yake kujifungua mtot wa kwanza.

Jacky Vicky katika mahojiano na Massawe Japanni
Jacky Vicky katika mahojiano na Massawe Japanni

Mwigizaji Jacky Vike almaarufu kama Awinja kutokana na kipindi cha Papa Shirandula alikuwa mgeni wetu siku ya Alhamisi katika kipindi cha Bustani la Massawe, kitengo cha Ilikuaje.

Akiwa kwenye mahojiano na Massawe Japanni, Jacky alifunguka kuhusu masuala mbalimbali kuhusu maisha yake ikiwemo familia na mahusiano yake.

Jacky alisema kuwa ana mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka minne ambaye kwa sasa amejikita katika kumpa malezi bora zaidi.

"Mwanangu ana miaka minne saa, atahitimu miaka mitano mwezi Juni. Kwa sasa nafurahia raha ya upande huo, sio ya uzazi. Wacha tutafutie mtoto karo ya shule. Kazi ya kulea sio rahisi" Jacky alisema.

Malkia huyo ambaye aliigiza kama kijakazi katika kipindi cha Papa Shirandula aliweka wazi kwamba bado hajawazia kupata mtoto wa pili.

Jacky hata hivyo alifichua kuwa ndoto yake ilikuwa kupata angalau watoto sita, wazo ambalo lilibadilika baada yake kujifungua mtot wa kwanza.

"Nilikuwa nimesema nitapata watoto sita. Hiyo ilikuwa kabla hata sijabeba ujauzito wa mwanangu, wacha nipate mtoto wa kwanza nione kulea sio rahisi! Nilisema nijikute! Sita, kwani wameagizwa wapi" Jacky alisema.

Mwigizaji huyo pia alifichua kwamba kufikia sasa amewahi kuwa kwenye mahusiano na wanaume watatu.