Ningependa uje uwe katika maisha ya mwanao- Carol Muthoni amwambia Mulamwah

Muhtasari

•Mwigizaji huyo alisema drama nyingi za hivi karibuni kati yake na Mulamwah zimetokana na hali  kuwa kila mmoja wao hajakubali kwamba walitengana.

•Muthoni alifichua kuwa mara ya mwisho kwa Mulamwah kuona mtoto wao ni akiwa na miezi miwili tu.

Carrol Sonnie katika studio za Radio Jambo
Carrol Sonnie katika studio za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO

Mwigizaji Caroline Muthoni alipotembelea studio zetu siku ya Jumatatu alizungumza mengi kuhusu mahusiano yake na mchekeshaji Mulamwah.

Akiwa kwenye mahojiano na Massawe Japanni, Muthoni alilaani madai ambayo mpenzi huyo wake wa zamani aliibua dhidi yake hivi majuzi.

Muthoni hata hivyo aliweka wazi kwamba hayuko tayari kujibu madai ya mchekeshaji huyo kutokana na heshima kubwa aliyo nayo kwake pamoja na binti yao. Alimuomba mpenzi huyo wake zamani kuwa na heshima pia.

"Ukweli ni kuwa mimi na yeye pekee ndio tunajua ukweli. Jambo bora zaidi ni kila mtu anyamaze tupeane heshima tu. Mimi nalilia heshima tu, hasa kwa mtoto. Tusianze kuvutana kwa  mtandao kwa sababu haitakuja kutatua tofauti zetu. Ni sisi wawili tu," Muthoni alisema.

Mwigizaji huyo alisema drama nyingi za hivi karibuni kati yake na Mulamwah zimetokana na hali  kuwa kila mmoja wao hajakubali kwamba walitengana.

Muthoni alisema hafahamu machungu ambayo baba huyo wa mtoto wake anayo dhidi yake huku akimuomba akubali kusonga mbele na maisha yake na kuangazia malezi ya mtoto wao tu.

"Kama tumekubaliana kusonga mbele, tuendelee mbele na maisha yetu tu.  Tukubaliane kuwa ambaye ametuleta pamoja ni Keilah. Haya machungu yote ambayo tuko nayo tuyabadilishe yawe upendo kwa Keilah, isikuwe vita kila wakati. Mi ningependa tuangazie Keilah badala ya yaliyopita kwa kuwa kila mtu alishasonga mbele," Alisema.

Mama huyo wa mtoto mmoja aliweka wazi kuwa hana kinyongo chochote dhidi ya mpenzi huyo wa zamani.

Alikiri kuwa anampeza mchekeshaji huyo huku akimsihi ahusike zaidi katika maisha ya binti yao wa miezi mitano.

"Tenga wakati uje uone mtoto wako, anaendelea vizuri. Ningependa uje uwe katika maisha yake. Uko karibu kila wakati. Hatukukatazi kuja kuona mtoto. Unajua kwangu ni kwako pia. Usijihisi umetengwa," Muthoni alisema.

Muthoni alifichua kuwa mara ya mwisho kwa Mulamwah kuona mtoto wao ni akiwa na miezi miwili tu.

Alisema kuwa kwa sasa anaishi kwa wazazi wake na anaangazia kazi na malezi ya binti yake tu. Alisema kuwa hana mpango wa kujitosa kwenye mahusiano mengine kwa sasa.