"Ni mimi nilianzisha talaka!" Willis afunguka kuvunjika kwa ndoa yake na Marya Prudence

"Ilikuwa chungu sana. Sio kitu ambacho ningetakia mtu yeyote!" alisema.

Muhtasari

•Katika mahojiano na Massawe Jappani, mtangazaji huyo alikiri kwamba yeye ndiye aliyeanzisha mchakato wa talaka hiyo.

•Pia alidokeza kuwa kumbukumbu za ndoa hiyo yake iliyovunjika huwa zinamsumbua mara kwa mara.

Willis Raburu katika studio za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO

Mtumbuizaji wa kipindi cha 10/10 kwenye Citizen TV Willis Raburu amefunguka kuhusu talaka yake na aliyekuwa mkewe Marya Prudence.

Katika mahojiano na Massawe Jappani, mtangazaji huyo alikiri kwamba yeye ndiye aliyeanzisha mchakato wa talaka hiyo.

"Heshima yote kwake. Yote tulisuluhisha mahakamani na tukaachana vizuri.Mimi niko sawa," alisema katika kitengo cha Ilikuaje?

Raburu hata hivyo alikiri kuwa hatua ya kutengana na mke huyo wake wa zamani iliumiza moyo wake sana.

"Ilikuwa chungu sana. Sio kitu ambacho ningetakia mtu yeyote!" alisema.

Aliongeza, "Hakuna mtu ambaye huingia kwa ndo akitazamia kutoka. Wakati fulani tulijipoteza."

Pia alidokeza kuwa kumbukumbu za ndoa hiyo yake iliyovunjika huwa zinamsumbua mara kwa mara.

Licha ya kutengana kwao, mtangazaji huyo alibainisha kuwa ataendelea kudumisha heshima yake kwa Bi Prudence.

"Nitamheshimu kwa sababu yeye ni mama wa mtoto wangu."

Raburu alikiri kuwa alikuwa na mchango katika kuvunjika kwa ndoa yake. Hata hivyo hakuweka wazi sababu halisi za kutengana na Prudence.

"Wakati mwingine nilijisahau kidogo. Nilijipoteza na kupoteza hisia. Hiyo ilipelekea mambo mengine ambayo hatimaye yalitutenganisha," alisema.

Raburu na Prudence walitengana mapema mwaka wa 2020 na kuanzisha mchakato wa talaka. Wawili hao walikuwa wamefunga pingu za maisha mwaka wa 2017 katika hafla iliyohudhuriwa na wanafamilia na marafiki kadhaa.