Nilisoma miezi 2 tu na kufanya mtihani wa KCPE na nakwenda Alliance Boys - Nuru Okanga

“Niliacha shule nikaanza kuchunga ng’ombe, nilikuwa nalipwa shilingi elfu moja na baadae elfu 3 na kisha nikaamia ukambani sehemu inaitwa Konza kuchunga kondoo, huko nilikuwa nafanyia 8,500."

Muhtasari

• Okanga mwenye umri wa miaka 32 alisema kwamba kilichofanya hakusoma mapema akiwa mdogo ni kutokana na kifo cha babake.

• Okanga alisema babake alifariki yeye akiwa na miaka 6 tu na yule ambaye aliachiwa majukumu ya kuwalea na kuwasomesha alikwepa na hapo ndipo aliacha shule ili kujukumikia familia.

Nuru Okanga
Nuru Okanga
Image: Facebook

Mtetezi mkali wa sera za Raila Odinga, Nuru Okanga amefichua kwamba aliketi darasani miezi miwili tu kabla ya kukalia mtihani wa KCPE wa mwaka 2023.

Akizungumza na mtangazaji Massawe Japanni katika stesheni ya Radio Jambo kwenye kitengo cha Ilikuaje, Okanga hata hivyo alisitasita kufichua alama alizozipata lakini akasema kwamba aliamua kurudi shuleni kwa sababu kuu mbili.

“Mimi nilisoma miezi miwili tu na nikafanya mtihani wa KCPE, niliamua kurudi shule kwa sababu ninalenga kuwa MCA lakini pia nilitaka nisije kuwa kiongozi ambaye hana cheti chochote cha masomo,” alisema.

Okanga mwenye umri wa miaka 32 alisema kwamba kilichofanya hakusoma mapema akiwa mdogo ni kutokana na kifo cha babake.

Okanga alisema babake alifariki yeye akiwa na miaka 6 tu na yule ambaye aliachiwa majukumu ya kuwalea na kuwasomesha alikwepa na hapo ndipo aliacha shule ili kujukumikia familia.

“Niliacha shule nikaanza kuchunga ng’ombe, nilikuwa nalipwa shilingi elfu moja na baadae elfu 3 na kisha nikaamia ukambani sehemu inaitwa Konza kuchunga kondoo, huko nilikuwa nafanyia 8,500. Nikaona huu ni upuzi nikaachana na hiyo kazi nikakuja hapa Nairobi. Nilianza kuchunga ng’ombe nikiwa na miaka 10. Nilitoka ukambani 2013 na nikakuja Nairobi nikaanza kufanya mjengo,” Okanga alisema.

Baadae pia alisema kwamba Nairobi alifanya kazi ya uchungaji katika eneo la Kayole, akisema kwamba alikuwa na ufahamu wa Biblia kichwani.

“Nilihubiri miaka 4, hakuna siku ungenipata nimeketi chini wikendi eti nachambua Biblia, maandiko yalikuwa yanakuja moja kwa moja kichwani,” Okanga alisema huku akitaja Zaburi kuwa kifungu chake pendwa.

Okanga alisema alibatizwa na kuitwa jina Paulo.

Okanga alifurahia Babu Owino kumpa ufadhili na akadokeza kwamab anaenda shule ya kitaifa ya Alliance Boys na akatuma ujumbe kwa mwalimu mkuu kwamba kila wikendi atakuwa anamuachia nafasi ya kwenda nyumbani kwani ana mke na mtoto.