"Nam'miss sana Chira!" Tiktoker shoga, Jude Magambo afunguka uhusiano wake na Brian Chira

Mwanatiktok huyo alifichua kuwa tayari yuko kwenye uhusiano na mwanaume mwingine.

Muhtasari

•Alisema licha ya kwamba marehemu alitangamana naye kimapenzi hasa walipokuwa kwenye sehemu za burudani, hawakuwahi kufikia hatua ya kuchumbiana.

•Katika mahojiano hayo, Magambo alikiri kuwa yeye ni shoga na kuwataka watu wamkubali jinsi alivyo.

Jude Magambo na marehemu Brian Chira
Image: HISANI

Mtayarishaji wa maudhui maarufu wa Kenya Jude Magambo almaarufu Manzi wa Meru amekanusha kuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na marehemu Brian Chira.

Akizungumza katika mahojiano na mtangazaji Massawe Japanni kwenye Radio Jambo, mwanatiktok huyo shoga aliweka wazi kuwa yeye na Chira walikuwa marafiki wakubwa tu.

Alisema licha ya kwamba marehemu alionekana kutangamana naye kimapenzi hasa walipokuwa kwenye sehemu za burudani, hawakuwahi kufikia hatua ya kuchumbiana.

“Hapana, sikuchumbiana naye. Ingawa, alikuwa mguso sana haswa wakati amelewa. Lakini hatukuwahi kuwa na mazungumzo hayo ya kuchumbiana,” Jude Magambo alisema.

Aliongeza, "Alikuwa anastarehe nami, na mwenye kugusana sana. Singemwambia aache, ningemruhusu kwa sababu nilijua ni pombe na wakati fulani ataacha. Lakini hatufiki hatua hiyo ya kuchumbiana.”

Mwanatiktok huyp hata hivyo alibainisha kwamba watu wengi wanaamini kwamba walikuwa wakichumbiana, na kudai kwamba wengine sasa hata wanamwita mjane.

"Kwangu mimi sikuchumbiana na Chira," alisema.

Magambo pia alikiri kumkosa sana marehemu Chira.

Alifichua kuwa marehemu tiktoker huyo alipokuwa hai, walifanya mambo mengi pamoja na kutengeneza kumbukumbu zisizofutika zinazomsumbua hadi sasa.

“Nimem’miss sana Chira. Na nilikuwa nikishiriki naye mambo mengi. Wakati fulani, alikuwa kama ndugu yangu. Wakati ambapo naskia ako mbali, nilikuwa naskia kuna kitu kisicho sawa.

Haikuwa inaisha hadi wiki moja kama sijamuaona, ama siku tatu,” alisimulia.

Alisema kuwa alikuwa akikutana na marehemu mara kwa mara hata baada ya kuhama kutoka walipokuwa wakiishi pamoja hadi Ruaka.

“Sasa napata wikendi imefika hivi nashindwa sasa Chira angekuwa hapa, tungekuwa mahali. Kila nilipotoka nae, nilihakikisha amefika nyumbani salama, juu namjua. Chira ni mtu akilewa alikuwa anasumbua sana, anavuruga,” alisema.

Alisema kuwa yeye na Chira walikuwa hawatengani kwani walikuwa wameanzisha urafiki mkubwa.

Katika mahojiano hayo, Magambo alikiri kuwa yeye ni shoga na kuwataka watu wamkubali jinsi alivyo. Pia alifichua kuwa tayari yuko kwenye uhusiano na mwanaume mwingine.