Nashukuru mume wangu hakuniacha- Evelyn Wanjiru azungumzia uchungu wa kukosa mtoto miaka kumi

"Nilipogundua ujauzito nilianguka chini, nikajawa na makamasi" Wanjiru alisema

Muhtasari

•Wanjiru alifichua kuwa suala la kutokuwa na mtoto lilianza kumsumbua baada ya kuwa kwa ndoa kwa miaka sita.

•Wanjiru amesema alisubiri mtoto kwa  muda mrefu hadi kufikia hatua ya kukata tamaa ya kuomba kupata mmoja

Image: INSTAGRAM// EVELYN WANJIRU

Mwimbaji wa nyimbo za injili Everlyn Wanjiru amefunguka kuhusu uchungu aliopitia katika kipindi kirefu ambapo alifanya majaribio mengi ya kupata mtoto bila mafanikio.

Akizungumza katika kipindi cha Bustani la Massawe, Wanjiru alisema ilimchukua mwongo mmoja kwenye ndoa ili kupata ujauzito wake wa kwanza.

Alifichua kwamba suala la kutokuwa na mtoto lilianza kumsumbua baada ya kuwa kwa ndoa kwa miaka sita.

"Baada ya miaka sita nilianza kushangaa mbona sipati watoto. Mwezi wangu ungepotea kwa kipindi cha miezi mitatu hadi miezi minne. Nilienda hospitalini nikapatiwa dawa ili mwezi wangu uje kwa wakati," Wanjiru alimwambia Massawe Japanni.

Mwanamuziki huyo alisema alianza kupatwa na wasiwasi baada ya kuona kuwa yeye na mume walikuwa wanazeeka.

Alikiri kwamba iliumiza sana moyo wake kuona hakuwa na uwezo wa kumtimizia mumewe furaha ya kuwa baba.

"Mume wangu alikuwa anatimiza miaka 40. Alikuwa anaona wenzake wana watoto ilhali yeye hana.. Nilikuwa naskia uchungu sana kwa sababu sikuwa na uwezo wa kumpatia mtoto. Vile nilitimiza miaka 30 nilihisi uwoga sana. Huo ndo wakati moyo wangu ulitishika," Alisema.

Wanjiru alisema mumewe ndiye aliyemtia moyo waende hospitalini kwa ajili ya kupimwa na kupokea matibabu.

Alieleza kwamba alitumia dawa za kurekebisha hali yake ya kukosa  usawa wa homoni kwa kipindi cha takriban miaka miwili.

"Daktari alikuwa ananiambia nitumie dawa kwa miezi sita. Miezi sita ikiisha bado sikuwa napata mimba. Daktari alitaka nitulie lakini singeweza kutulia, nilitaka mtoto," Alisema.

Mwimbaji huyo aligundua kuhusu ujauzito wake mwaka jana wakati ambapo alikuwa katika ziara nchini Marekani.

Habari hizo zilimsisimua moyo wake sana ila hakujua jinsi ya kusherehekea kwani alikuwa amesubiri kwa muda mrefu.

"Nilichukua kifaa cha kupima nikaingia kwa choo, nikapima nikawekelea kifaa hicho kwa sink nikaendelea kutumia simu kwani tayari nilikuwa nimeona mstari mmoja. Baadae nilichukua kifaa hicho ili kukitupa lakini nikaona laini mbili. Nilianguka chini, nikajawa na makamasi na machozi," Alisema.

Wanjiru alibarikiwa na mtoto wake wa kiume mwezi Aprili mwaka huu. Mtoto huyo alipatiwa jina  Mshindi Akweyu Agundabweni.

Wanjiru amesema alisubiri mtoto kwa  muda mrefu hadi kufikia hatua ya kukata tamaa ya kuomba kupata mmoja. Pia alikata nywele zake baada ya kuchoka kungoja mtoto.

"Nashukuru Mungu kwa kunipa mume ambaye hakuniacha.. Ni kitu kizuri kupata ujauzito, ni kitu kizuri kuitwa mama," Wanjiru alisema.

Mwanamuziki huyo amemshukuru Mola kwa kutimiza maombi yake licha ya miaka mingi ambayo ilichukua.