Mbusii na Lion wafichua mishahara yao ya kwanza na jinsi walivyoitumia

“Kwanza nililipa nyumba. Nikabaki na change. Nikatoa lock. Niliskia raha sana," Mbusii alisema.

Muhtasari

•Lion aliweka wazi kuwa pesa nyingi zaidi alizopokea mara ya kwanza baada ya kazi ya mwezi mmoja zilikuwa Ksh 20,000.

•Mbusii alifichua kuwa alitumia mshahara wake wa kwanza kulipa kodi ya nyumba na kujiburudisha.

Watangazaji Lion na Mbusii

Watangazaji wa kipindi cha Mbusii na Lion Teke Teke kwenye Radio Jambo Daniel Githinji Mwangi (Mbusii) na  Cyrus Afune (Lion) wamefunguka kuhusu mishahara yao ya kwanza.

Katika mahojiano na mwandishi Caroline Mbusa, Wawili hao ambao wamekuwa wakifanya kazi pamoja kwa miaka mingi walifichua kwamba wote wawili walipata mishahara yao ya kwanza katika siku za ujana wao mdogo.

Lion aliweka wazi kuwa pesa nyingi zaidi alizopokea mara ya kwanza baada ya kazi ya mwezi mmoja zilikuwa Ksh 20,000.

"Nilipata 20,000 nikashangaa kama ni zangu. Mshahara ya kwanza ndiyo huwa na athari zaidi. Hiyo siku Umoja yote walijua mimi ni mtoto wa Chairman!" alisema.

Mtangazaji huyo wa reggea hata hivyo alidokeza kuwa kwa sasa tayari amezoea kupokea pesa nyingi na amejifunza jinsi ya kuzitumia kwa busara.

Hadithi ya mwenzake Mbusii sio tafauti sana ila yeye alipokea kiasi cha chini zaidi yake kama mshahara wa kwanza. Kwa upande wake, Mbusii alipokea shilingi 5,000 tu kama malipo yake ya kwanza ya mwezi.

"Nilishika elfu tano. Wakati huo nilikuwa hali mahututi. Nilipopata hiyo elfu tano, ni kama ilikuwa imebarikiwa. Baada ya hapo kalianza kutamba," alisema.

Mtangazaji mkuu huyo wa kipindi cha jioni alifichua kuwa alitumia mshahara wake wa kwanza kulipa kodi ya nyumba na kujiburudisha.

“Kwanza nililipa nyumba. Nikabaki na change. Nikatoa lock. Niliskia raha sana," 

Wawili hao pia walifunguka kuhusu kufanya kazi pamoja. Walisema kuwa imekuwa safari ya kusisimua sana kutangaza pamoja, si tu kwa sababu ni wafanyakazi wenza lakini pia kwa sababu wao ni marafiki wakubwa.

"Mi nahisi vizuri kwa sababu nafanya kazi na rafiki yangu. Ni rahisi kama unafanya kazi na rafiki yako. Ni mrasta na mimi ni mrasta, unasoma dini moja, tulilelewa Eastlands, inakuwa ni rahisi kushirikiana," Lion alisema.

Lion alibainisha kuwa hata katika ulimwengu mwingine angechagua kufanya kazi na mtangazaji huyo mwenzake.

Mbusii kwa upande wake aliweka wazi kuwa ni rahisi kufanya kazi na Lion kwa sababu wana muungano mzuri.

"Huyo ni bro. Kuchapa kazi naye ni rahisi. Hakuna kufanya mazoezi. Kinachokuja akilini, tayari sisi ni tunaelewa," alisema.

Wawili hao hutangaza shoo ya jioni ya Radio Jambo kuanzia saa tisa jioni hadi saa moja jioni, Jumatatu hadi Ijumaa.