Nikitoka nje ya line, Gidi hunirejesha kama Mwalimu Mkuu- Ghost afunguka kufanya kazi na Gidi

Ghost alibainisha kuwa mara zote Gidi huwa tayari kumrekebisha kila anapokosea.

Muhtasari

•Ghost alibainisha kuwa ni mara chache tu  ametofautiana na Gidi kwa miaka kumi na minne iliyopita ambayo wamekuwa wakifanya kazi pamoja.

•Aliweka wazi kuwa yeye kwa ujumla ni mtu mwenye furaha na kicheko chake ni cha kweli na cha asili.

ndani ya studio za Radio Jambo.
Mtangazaji Jacob Ghost Mulee ndani ya studio za Radio Jambo.

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Jacob 'Ghost' Mulee ameweka wazi kuwa kufanya kazi kama mtangazaji mwenza wa Gidi imekuwa ni safari nzuri ya kufarahisha.

Katika mahojiano na mwandishi Samuel Maina, Ghost alibainisha kuwa ni mara chache tu  ametofautiana na Gidi kwa miaka kumi na minne iliyopita ambayo wamekuwa wakifanya kazi pamoja.

"Tumefanya kazi vizuri kwa miaka kumi na nne bila wasiwasi wowote.  Hakuna kukorofishana, huwa ni masuala ya kazi, kama kuna tofauti huwa za kikazi na baada ya pale tunatoka tunaenda zetu," alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars alilinganisha uhusiano wake wa kikazi na Gidi na ndoa imara.

Hata hivyo, amekiri kuwa kama ndoa nyingine yoyote, hakujakosa changamoto katika 'ndoa' yake na mtangazaji huyo. Alibainisha kuwa mara zote Gidi huwa tayari kumrekebisha kila anapokosea kazini.

"Ni ndoa ambayo huwezi kuiacha isipokuwa uamue hivyo. Tumekaa kwa hii ndoa miaka kumi na minne. Imekuwa ni changamoto. Gidi ana haiba tofauti na yangu. Lakini nampenda kwa sababu tukifanya naye kazi, unapata saa zingine mimi ni mtu wa mzaha, nikitoka laini ananirejesha kama mwalimu mkuu," alisema.

Ghost alizungumzia kitengo maarufu kwenye kipindi chao 'Patanisho' na kusema kuwa inawapa furaha nyingi kusaidia watu kurudiana.

"Ni raha yetu waliokosana wakiweza kupatana na kurudiana. Hakuna haja ya kukaa na kinyongo moyoni. Kama umekosea mtu muombe msamaha. Kama amekukosea nawe kubali msamaha," alisema.

Mtangazaji huyo pia alizungumzia kicheko chake ambacho ni utambulisho wake na huwavutia mashabiki wengi wa Radio Jambo.

Aliweka wazi kuwa yeye kwa ujumla ni mtu mwenye furaha na kicheko chake ni cha kweli na cha asili.

"Ni kicheko changu halisi. Mimi ni mtu wa furaha na kawaida wangu napenda kucheka. Napenda kucheka wakati wote, nikikasirika labda sekunde moja," alisema.