Jamaa aliyejitambulisha kama Francis Orondo ,31, kutoka Nakuru alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Mama Vanessa ,28, ambaye alikosana naye hivi majuzi.
Francis alisema ndoa yake ya miaka mitatu ilivunjika wiki jana wakati alipotoka kazini na kupata mkewe amehama na kila kitu.
"Wiki jana Jumatano nilipata amebeba vitu za nyumba akaenda kukodisha nyumba yake. Shida ilikuwa ni mambo tu ya nyumba, mambo ya kukosa pesa. Pia anasema sipendi mtoto wake ambaye alikuja naye. Mtoto akifanya kosa, nikimkosoa anasema namchukia. Aliniambia eti ashapata mtu, sijui kama ni kunichezea," Francis alisema.
Aliongeza, "Mimi nilikuwa natoa pesa ya matumizi kwa nyumba wakati nikipata. Lakini nafanya kazi ya juakali na siku hizi hakuna pesa.Sijatembea kwao. Ndo nilikuwa napanga hii mwaka Mungu akinijalia niende kwao."
Francis alisema haamini madai ya mkewe kwamba amepata mtu mwingine.
"Hiyo ni kama tu kunishtua roho," alisema.
Juhudi za kumpatanisha Francis na mkewe hata hivyo hazikufua dafu kwani Mama Vanessa likuwa amezima simu yake.
Katika ujumbe wake wa mwisho kwa mkewe, Francis alimwambia, "Naomba tu urudi tuendelee na maisha kabla Mungu atupee njia. Sina ubaya wowote na mtoto wako, wote ni wangu.'
Je, una ushauri ama maoni gani kuhusu Patanisho ya leo?