Jamaa aliyejitambulisha kama Douglas Bassam ,24, kutoka Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na baba yake mzazi Martin Nyongesa Wanyama ,45, ambaye alikosana naye mwishoni mwa mwaka jana.
Douglas alisema uhusiano wake na babake uliharibika Desemba mwaka jana wakati alipozozana naye hadi kumkata na panga.
"Ilikuwa tu mambo na mizozo ya nyumbani, tuligombana na baba alafu kidogo nikashtukia nimemkata kwa kichwa. Alitaka kunifunga nikatoroka nikawa narandaranda," Douglas alisimulia.
Aliendelea, "Sasa hivi niko tu kwa hii mtaa yangu lakini nimejificha. Watu wa nyumbani hawajui mahali niko. Niliskia wananitafuta na polisi nikatoroka. Saa hii niko mahali pabaya sijielewi. Nilimkata tu vibaya kwa kichwa."
Douglas alisisitiza kwamba, licha ya kumjeruhi vibaya babake, ana uhakika kwamba yuko hai bado kwani hajaskia matanga yoyote.
Alipoulizwa chanzo cha mzozo wake na mzazi huyo wake, alidai kwamba alibishana naye kuhusu maji ya ugali.
"Ilikuwa tu mambo na ugali, walipunguza maji ya ugali nikaleta shida," alisema.
Bw Martin alipopigiwa simu alifichua kwamba mwanawe alikuwa akitembea na marafiki wabaya na alitumia mihadarati.
"Ilikuwa mwaka jana Disemba. Alikuwa anatembea na marafiki zake wengine. Alikuwa anatumia pombe, sigara, bangi. Mpaka akanikata kwa kichwa.
Sijui mahali yuko. Huwa naskia na marafiki zake eti huwa anapatikana usiku. Alitaka kunimaliza," Martin alisema.
Douglas alijaribu sana kuomba msamaha akiashiria majuto yake ila juhudi zake zilionekana kuangulia patupu.
"Wakati ulikuwa unakuja nyumbani unanigombanisha mimi na mama yako, ulikuwa unafikiria nini? Umeachana mambo na pombe? Na sigara? Umeachana na hao marafiki zako ambao huwa unatembea nao?" Martin alimuuliza mwanawe.
Douglas alikiri kuacha pombe na sigara ila akaweka wazi kwamba bado hajaachana na marafiki zake.
"Hiyo ni kama tu unataka kunimaliza. Saa hii niko na alama kwa kichwa, ata sina pesa ya kuenda hospitali," Martin alisema.
Aliongeza, "Saa hii siwezi kusamehe, wewe ulikuwa na chaguo. Labda ukuje nyumbani tuongee. Nilikuwa nishapeleka ripoti kwa polisi."
Douglas alimwambia, "Ndio nilikosea, lakini naomba msamaha. Nikija nyumbani si utanifunga?"
Bw Martin hata hivyo alishikilia msimamo wake akisema, "Siwezi kumsamehe saa hii juu ya mambo ambayo alinifanyia. Aendelee kukaa mahali yuko. Nilikuwa nimepeleka ripoti kwa polisi. Asirudi nyumbani."
Je, una maoni yepi kuhusu Patanisho ya leo?