Patanisho:'Pia mimi niko na mke' Jamaa adai baada ya aliyekuwa mkewe kufichua anaolewa kwingine Desemba

Mwanamke huyo alisema kuwa Simiyu alikuwa anadanganya kusema kuwa walikuwa kwenye uhusiano thabiti na hakueleza sababu zilizosababisha kukosana kwao.

Muhtasari

•Jamaa mmoja alituma ombi kupatanishwa na mkewe ambaye alidai walitengana mapema mwakani baada yake kuhamia Nairobi kwa sababu za kikazi.

•Simiyu alidai kuwa Mercyline alikataa kujiunga naye Nairobi  akidai kuwa hangewezana na hali ya anga jijini.

•Cha kustaajabisha zaidi ni kwamba Mercyiline alifichua kuwa alikuwa anakusudia  kufunga ndoa na mwanaume  mwingine mwezi Desemba

Ghost na Gidi
Image: Studio

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha patanisho alfajiri ya Jumanne, jamaa mmoja alituma ombi kupatanishwa na mkewe ambaye alidai walitengana mapema mwakani baada yake kuhamia Nairobi kwa sababu za kikazi.

Jack Simiyu alidai kuwa alikuwa ameahidi mkewe Mercyline kuwa baada ya kufanikiwa kazini angemtumia nauli  ajiunge naye jijini ila baada ya wiki kadhaa mazungumzo yao yakaanza kubadilika. 

Simiyu alidai kuwa Mercyline alikataa kujiunga naye Nairobi  akidai kuwa hangewezana na hali ya anga jijini.

"Nilikuja kazi Nairobi na nikaambia bibi yangu kuwa nikipata pesa ningemtumia pia naye aje jijini. Ile harakati ya kuja Nairobi, kumpigia simu akaanza kuniambia kuwa hali ya anga ya Nairobi hawezani nayo. Baada ya hapo nikimpigia simu akaanza kukata simu zangu na akaniblock" Simiyu alisimulia.

Mercyline alipopigiwa simu alipuuzilia mbali uhusiano wowote na Jack na kudai kuwa hamfahamu.

"Simjui! Hata sitaki kusikia. Mimi hata simjui wacaneni na mimi. Muulize alikuwa anataka nini, mimi simjui! Muulize alinikosea aje?" Mercyline alisema.

Simiyu alieleza kuwa alihitaji kusaidiwa kumfikia aliyekuwa mpenzi wake kwa sababu hakuwa anashika simu zake kila alipopiga.

Mercyline kwa upande wake alisema kuwa alikuwa amemsamehe ila hakutaka uhusiano wowote na jamaa huyo kwani alikuwa ashasonga mbele na maisha yake. Alisema kuwa hakuwahi kuwa na uhusiano wowote na Simiyu.

"Ni Mungu tu anajua. Hatukuwa na uhusiano wowote na yeye.. Sijui, aachane na mimi kabisa. Na anasema eti anataka kuzungumza nami aniombe msamaha. Anajua kweli nilivyoteseka kwa sababu yake?" Mercyline alisema.

Mwanamke huyo alisema kuwa Simiyu alikuwa anadanganya kusema kuwa walikuwa kwenye uhusiano thabiti na hakueleza sababu zilizosababisha kukosana kwao.

Cha kustaajabisha zaidi ni kwamba Mercyiline alifichua kuwa alikuwa anakusudia  kufunga ndoa na mwanaume  mwingine mwezi Desemba

"Mwambie amekosea kwa sababu naolewa mwezi wa Desemba. Mwambie asiifanye kuwa suala kubwa. Sijui kama anayetaka kunioa anasikiza" Alidai.

.Kuskia hayo Jack naye aliamua kubadilisha msimamo wake na kudai kuwa tayari alikuwa ameoa mke mwingine na alitaka tu kuomba msamaha kwa yale alikuwa ametenda.

"Nilitaka kumwambia vile nilimwambia aje Nairobi akakataa hata mimi nishaoa niko na mke tayari. Kwa hivyo nilikuwa tu nataka kumuomba msamaha,. Nilikuwa nataka turejeane lakini vile ashasonga mbele na maisha yake pia mimi nimeoa niko na bibi" Jack alidai.