Patanisho: "Alinionya nisibebe wanadada sana" Mwendesha bodaboda aeleza masaibu yaliyokumba ndoa ya miaka 7

Bwana Dickson alidai kuwa walitengana na mkewe mnamo Juni 2018 baada ya kutofautiana kuhusu masaa ya kuingia kwa nyumba

Muhtasari

•Dickson alisema kuwa kazi yake ya kuendesha bodaboda ilikuwa inamfanya aingie kwa nyumba akiwa amechelewa sana, jambo ambalo halikupendeza mkewe.

•Margaret alikanusha madai kuwa walitengana kufuatia mzozo kuhusiana na masaa ya Dickson kurudi kwa nyumba na kudai kuwa sababu yake kuu kuondoka pale ni baada yake kusingiziwa kuwa alihusika katika mauaji ya mama mkwe.

•Kwa upande wake Margaret alisema kuwa hawezi kumrudia aliyekuwa mumewe kwani alikuwa ashasonga mbele na maisha yake.

Ghost na Gidi
Image: Studio

Kwenye kipindi chetu cha Gidi na Ghost  asubuhi ya leo (Agosti 12)  kitengo cha Patanisho, Dickson Ambonyi kutoka Voi alitaka kupatanishwa na bibi wake wa miaka saba ambaye walikosana na mke wake Margaret  ambaye walikosana mwaka wa 2018.

Bwana Dickson alidai kuwa walitengana na mkewe mnamo Juni 2018 baada ya kutofautiana kuhusu masaa ya kuingia kwa nyumba.

Jamaa huyo alisema kuwa kazi yake ya kuendesha bodaboda ilikuwa inamfanya aingie kwa nyumba akiwa amechelewa sana, jambo ambalo halikupendeza mkewe.

Dickson pia alisema kuwa mkewe alikuwa amempatia ilani dhidi ya kubeba wanawake kwa pikipiki yake.

"Ilifika mahali akawa ananiambia nikiwa kwa stage kubeba wateja nisibebe wanadada sana.. tulikuwa tunasumbua juu ya mambo kidogo kidogo" Dickson alisema.

Alisema alishtukia asubuhi moja kupata mkewe akiwa amefunga  virago vyake na kuenda.

Juhudi za Dickson kujaribu kumsihi Margaret arudi nyumbani hazijawahi kufua  dafu kwa kipindi cha miaka mitatu ambayo wametangana.

Kwa upande wake Margaret alisema kuwa hawezi kumrudia aliyekuwa mumewe kwani alikuwa ashasonga mbele na maisha yake.

"Nilishasonga mbele na maisha.. yangu na yeye yaliisha, alinifnyia mambo mengi lakini yangu na yake yaliisha. Kwa sasa kazi yangu ni kutafutia watoto" Margaret alisema.

Mwanamke huyo alisimulia masaibu aliyopitia wakati alikuwa anamchumbia Dickson. Alisema kuwa alilazimika kuoleka mapema baada yake kupata ujauzito wakati alikuwa anapanga kujiunga na chuo kikuu.

"Huyo mwanaume achana na yeye.. unajua nilikuwa mjamzito na nilikuwa nijiunge na chuo kikuu. Sikuenda kwa sababu ya ujauzito wakanidanganya watanipeleka shule alafu wakanipeleka tu hivihivi wakaanza kunitesa wakanifanyia tu vitu mingi wakiwa na mama mkwe na dadake. Nilioleka nikiwa mdogo sana alinipotezea wakati" Margaret alisema.

Alifichua kuwa mumewe alikuwa mwenye vurugu na alikuwa anampatia vitisho vya kumdunga kwa kutumia chuma.

"Alikuwa anakaa na chuma kwa nyumba ananiambia atanidunga nayo eti atanikatakata.. hadi huyo mtoto mdogo na mwenye ako naye wanajua baba yao ni mbaya alikuwa anataka kunidunga na chuma" Margaret alisema.

Mwanadada huyo aliyesikika kajawa na ghadhabu alisema haja yake ilikuwa tu watoto wasome.

Margaret alikanusha madai kuwa walitengana kufuatia mzozo kuhusiana na masaa ya Dickson kurudi kwa nyumba na kudai kuwa sababu yake kuu kuondoka pale ni baada yake kusingiziwa kuwa alihusika katika mauaji ya mama mkwe.

"Alinidharau mpaka akaniambia hakuna mahali naweza enda. Sababu kubwa ni kwamba mamake aliaga na wakasema ni mimi nilimuua.. hiyo ingine nilikuwa navumilia lakini hiyo ilikuwa sababu kubwa yangu kuondoka. Ilifika mahali hata dada zake hawakuwa wanataka kuniona na hakukuwa kunakalika kwa nyumba. Hadi baba mkwe alianza kuniongelea na kusema kuwa mimi ni mbaya nikaona hakukaliki nikasema niondoke."  Alisema Margaret.

Alieleza kuwa hata familia yake ilimkataza kurudi kwa kina mume baada ya yale alipitia pale.

Hata hivyo, Dickson aliridhika kupata majibu aliyohitaji kuhusu msimamo wa aliyekuwa mkewe. Alisema kuwa amekuwa akijaribu kupata majibu ila Margaret hakuwa anamwambia ukweli.

Wawili hao walifanya maamuzi ya kusonga mbele na maisha kila mmoja wao.