Patanisho: "Najua ana mke mwingine ila ningependa turudiane" Mwanadada aliyetengana na mumewe 2018 aomba kumrudia

Alisema kuwa hana nia ya kuolewa mahali kwingine kwa kuwa ana watoto waliopata pamoja na aliyekuwa mumewe.

Muhtasari

•Adhiambo alidai kuwa ndoa yake ilivunjika mwaka wa 2018 baada ya mumewe kudai kuwa alisababisha afutwe kazi, madai ambayo mwenyewe anapuuzilia mbali.

•Victor alisema kuwa Adhiambo alipata ajali wakati alikuwa anatoroka na watoto kutoka nyumbani kwao ambako alikuwa amewapeleka kuishi na jambo hilo lilimkera.

Ghost na Gidi
Image: Studio

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha patanisho, mwanadada mmoja aliyejitambulisha kama Valentine Adhiambo alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Victor Wamalwa ambaye walitengana miaka mitatu iliyopita.

Adhiambo alidai kuwa ndoa yake ilivunjika mwaka wa 2018 baada ya mumewe kudai kuwa alisababisha afutwe kazi, madai ambayo mwenyewe anapuuzilia mbali.

"Tulikuwa tumekosana kwa sababu ya mambo ya kazi. Alikuwa anafanya kazi mahali. Kuna vile wakakosana pale kazini alafu akafutwa. Sasa vile alifutwa kazi ikawa ni mimi kisingizio ati nimeenda pale kazini nikamfuta.. sijawahi fanya kitu kama hiyo. Baadae nikatoka akanipeleka kwao. Baada ya hapo kisingizio ikawa nyingi mimi nikaondoka nikaenda zangu" Adhiambo alieleza.

Juu ya hayo, mwanamke huyo amedai kuwa mumewe alianza kujihusisha na mambo ya mpango wa kando na pia wakaaza kuzozona na mama mkwe.

Adhiambo alisema kwamba anafahamu kuwa kwa sasa mumewe ameoa mke mwingine ila angependa kurudi kuchukua tena nafasi yake kwa kuwa angataka wasaidaine kushughulikia watoto.

"Nilitoka huko kama ako na mtu.. mimi ndio nilikuwa wa kwanza akaleta mke mwingine.. Ningependa kurudi kwa sababu watoto ambao niko nao wananisumbua, wanaugua  maramara, mwingine akianza asubuhi mwingine jioni.. ningependa ashughulikie watoto kwa sababu nikimpigia simu anasema kuwa watoto wakipatikana na shida yoyote nitawakula" Adhiambo aliambia Gidi.

Mwanamke huyo alisisitiza kuwa angependa kurudiana na mumewe, sio tu kwa ajili ya watoto mbali pia kwa sababu anampenda sana.

Alisema kuwa hana nia ya kuolewa mahali kwingine kwa kuwa ana watoto waliopata pamoja na aliyekuwa mumewe.

"Hakuna vile naweza enda kivyangu na niko na watoto wake. Hata nikisema nataka kuolewa mahali kwingine hao watoto nani atawashughulikia?.. Nataka mtupatanishe kama atakubali turudiane tulee watoto wetu pamoja.. yeye ndo ataamua lakini mimi nataka turudiane. Kukaa pekee yangu na watoto sio vizuri. Watoto wanafaa kukaa na wazazi wake" Alidai Adhiambo.

Victor alipopigiwa simu alipuuzilia madai ya mkewe kuwa walitengana kwa sababu ya mambo ya kufutwa kazi. Alisema kuwa Adhiambo alitoroka mwenyewe bila kushurutishwa na yeyote kuenda.

Victor alisema kuwa Adhiambo alipata ajali wakati alikuwa anatoroka na watoto kutoka nyumbani kwao ambako alikuwa amewapeleka kuishi na jambo hilo lilimkera.

"Wewe ulitoroka na watoto kwa bahati mbaya watoto wakapata ajali na wewe unaelewa vile kulienda  mtoto alipopata ajali.. hukuwa umeniambia, ulitoka wakati nilikuwa kazi hukuniambia" Victor alimwambia Adhiambo.

Adhiambo kwa upande wake alijitetea kwa kusema kuwa aliondoka nyumbani kufuatia jumbe mbaya ambazo mumewe alikuwa anamtumia. Alimuomba mumewe kufika kwao ili wazungumze na wazazi wake warudiane. 

Victor alisema kuwa ako tayari kurudiana na mkewe baada yake kuenda kwao na kukubaliana na wazazi wake.

Alisema kuwa angejaribu sana kadri ya uwezo wake kuwa na wake wawili kwa kuwa kwa sasa ana mke mwingine.

"Niko tayari kabisa kurudiana naye.. niko na mke saa hii lakini yeye anajua ndiye alikuwa wa kwanza.. nitajaribu  kukaa na wake wawili. Nimekubali, sina mabaya na yeye. Ata ukimuuliza huwa nashughulikia watoto yeye ndiye huwa sishughulikii"  Alidai Victor.

Victor ambaye alisita kutaja kazi ambayo anafanya akihofia kuwa wanafamilia wake ambao wanafahamu kuwa anafanya kazi kwa ofisi walikuwa wanaskiza Radio Jambo alisema kuwa huwa anashughulikia watoto na ako na ushahidi wa jumbe za Mpesa.

"Niko na jumbe za pesa ambazo huwa natumia watoto.. saai natoka Malaba naenda Eldoret kikazi.. kwa saa hii siwezi kusema kazi nafanya.. mimi sio mwizi, mimi ni dereva.. unajua nyumbani wanasikiliza Radio Jambo saa hii na wanajua nafanya kazi kwa ofisi" Victor alisema.

Wawili hao waliambiana maneno matamu ya kumalizia na kuagana kuwa wanapenda na wangefanya mikakati ya kurudiana.