Patanisho: 'Mume wangu alinipiga na nyahunyo, aachane na mimi' Mwanadada asimulia alivyodhulumiwa na jamaa aliyemshuku kuwa na mpango wa kando

Wilfrida alisema kuwa Dennis alimkosea na kumdhalilisha sana na hataki uhusiano wowote na yeye tena.

Muhtasari

•Dennis,30 alidai kuwa walitengana na mkewe  Winfrida Omweke 26,  kufuatia mzozo 'kidogo' wa kinyumbani baada ya kuwa  kwa ndoa kwa kipindi cha miaka minne.

•Mwanamke huyo alimshauri Dennis ajifunze kuheshimu mkewe na kumtunza  ifaavyo iwapo ataamua kutafuta bibi mwingine. Alisema kuwa yeye hana nia ya kuolewa tena.

Ghost Mulee
Ghost Mulee
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, Bwana Dennis alituma Ombi kupatanaishwa na mkewe ambaye walitengana mwezi Septemba mwaka uliopita.

Dennis,30 alidai kuwa walitengana na mkewe  Winfrida Omweke 26,  kufuatia mzozo 'kidogo' wa kinyumbani baada ya kuwa  kwa ndoa kwa kipindi cha miaka minne.

Dennis alipigwa na butwaa kubwa aliporudi kutoka  kazini siku moja na kupata mkewe akiwa amefagia kila kitu kwa nyumba na kutoweka.

"Nilipata jumbe kwa simu yake walizokuwa wanaandikiana na jamaa mwingine tukazozana niliporudi kutoka kazini nikapata ametoroka. Alienda na kila kitu kilichokuwa kwa nyumba" Dennis alieleza masaibu yake.

Alisema kuwa juhudi za kumfikia mkewe tangu siku ile zimeangulia patupu kwani hajakuwa akichukua simu zake.

Dennis alifichua kuwa walipokuwa wanafunga ndoa mkewe tayari alikuwa na mtoto mmoja kutoka kwa uhusiano mwingine. Hata hivyo alisema kuwa alimpenda mtoto yule kama  kwamba alikuwa wake.

Ghost aliweza kumfikia Wilfrida ila mwanamke huyo aliyesikika kajawa na ghadhabu kweli hakutaka kumskia aliyekuwa mumewe hata kidogo.

Wilfrida alisema kuwa Dennis alimkosea na kumdhalilisha sana na hataki uhusiano wowote na yeye tena.

"Mwambie awachane na mimi na asahau kabisa. Sitaki kurudia alichokifanya.. Nilikuwa nafanya kazi na huo wakati hakuwa analipa nyumba. Ilifika mahali mwenye nyumba akasema amechoka akatwambia tutoke. Mwenye nyumba alipopigia Dennis simu alisema kuwa yeye alikuwa tayari ameshatoka na kuenda kwa msichana mwingine na akamwambia kuwa akitaka kututoa pale atufukuze.

Alikuwa ameambia ameambia majirani kuwa alikuwa ameshapata bibi na alikuwa anaenda kumuoa. Hata pesa nilizokuwa nimeweka pale kwa nyumba alichukua zote akaenda kwa huyo msichana.

Alikuwa amenichapa na nyahunyo hata watu wa ploti ndio waliniambia nitoke tu niende kwetu. Alinichapa na nyahunyo nikatoroka mpaka kwa bafu. Alikuwa  abomoe bafu. Alikalishwa chini aeleze shida yake ila hakuwa anasema. Hakuwa amekunya hata pombe alikuwa sawa. Sitakangi kabisa kukumbuka ile siku" Winfrida alisimulia.

Mwanamke huyo alimshauri Dennis ajifunze kuheshimu mkewe na kumtunza  ifaavyo iwapo ataamua kutafuta bibi mwingine. Alisema kuwa yeye hana nia ya kuolewa tena.

Dennis kwa upande wake alikanusha madai kuwa aliwahi kuambia majirani kuwa amepata mke mwingine ila alikubali kuwa alimgombeza mkewe kutokana na hasira.

Hata hivyo alisema kuwa alifurahia kujua msimamo wa Winfrida kwani sasa anaweza kufanya maamuzi ya kusonga mbele na maisha yake bila wasiwasi.