Patanisho:"Mke wangu aliniacha baada yangu kutumia pesa za chama kununua miwa" Jamaa asimulia masaibu yaliyokumba ndoa yake

Alieleza kuwa alimpiga mkewe walipokuwa wanazozana usiku kitenda ambacho kilimfanya apige simu nyumbani kwao asubuhi iliyofuata akakujiwa na ndugu zake wakarudi kwao

Muhtasari

•Shaban alieleza kuwa maamuzi yake yaliibua mzozo mkubwa kati yao ambao ulisababisha ampige mkewe kutokana na hasira hadi akatoroka na kurudi kwao.

•Jamaa huyo alisema kuwa baada ya miezi kadhaa mkewe alihamia Nairobi na kumuachia watoto watatu. Kufuatia hayo akaamua kuoa mke mwingine ili amsaidie kulea watoto.

ghost
ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho siku ya leo, Bwana Shaban Achesa kutoka Mumias alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Jackline Achesa ambaye walikosana mwaka wa 2019 baada ya kuwa kwenye ndoa kwa miaka tisa.

Kulingana na Shaban, ndoa yao ilivunjika baada ya kutofautiana kuhusu mambo ya pesa za chama ambazo mkewe alimpatia aweke ila yeye akaamua kuzitumia kununua mbegu za miwa ili apande.

Shaban alieleza kuwa maamuzi yake yaliibua mzozo mkubwa kati yao ambao ulisababisha ampige mkewe kutokana na hasira hadi akatoroka na kurudi kwao.

"Chama ilikuwa kwa nyumba yetu. Wakati wageni walienda akanipatia pesa niweke. Ilikuwa shilingi 6000. Wakati huo nilikuwa naendesha pikipiki. Nilichukua ile pesa nikaenda nikalipa mbegu za miwa mahali kwa kuwa nilikuwa nimelima shamba. Vile nilileta hizo mbegu watu wakaanza kupanda , nilpoenda akaenda shambani akafukuza hao watu. Wakati walinipigia simu nikiwa mbali nikarudi. Mchana sikuanza vita sana na yeye nikamuomba msamaha nikamwambia hiyo miwa ingemsaidia baadae. Akaniambia ningemwambia kwa sababu alikuwa anataka tununue mabati tujeke jikoni. Nikamwambia kweli nimekosa anisamehe.

Kumbe hiyo hasira yake haikuisha. Wakati  nilirudi jioni akanipea chakula vizuri nikaoga alafu tukaenda kulala. Hapo nikamuongelesha akaanza matusi bahati mbaya kwa kuwa hasira yangu ni ndogo nikamchapa nikamuumiza kidogo" Shaban alisimulia.

Alieleza kuwa kufuatia vita hiyo mkewe alipiga simu kwao asubuhi iliyofuata akakujiwa na ndugu zake wakarudi kwao.

"Baada ya kukaa kidogo nikaenda kwao akasema harudi kwa kuwa bado alikuwa na hasira. Ndugu zake ni kama walimpeleka hospitali na wakati huo sikuwa na pesa " Alieleza Shaban.

Jamaa huyo alisema kuwa baada ya miezi kadhaa mkewe alihamia Nairobi na kumuachia watoto watatu. Kufuatia hayo akaamua kuoa mke mwingine ili amsaidie kulea watoto.

Mkewe aliposikia kuwa Shaban alikuwa ameoa mke mwingine akafunga safari kutoka Nairobi na akaenda kuchukua watoto wake na akafukuza yule mke mwingine.

"Alikuja Desemba 27. Mimi nilikuwa kuona mpira. Niliposikia ako nyumba nikamwambia aningoje. Nilipoenda nikamwambia kuwa hawezi kuchukua watoto mpaka bibi mwingine akuwe kwani ni yeye alikuwa anawalinda. Kesho iliyofuata nilipoenda kazini kurudi nilipata ashachukua watoto na kufurusha yule mke mwingine" Shaban alieleza.

Shaban alisema kuwa babake alimuonya asiwahi oa bibi mwingine ila yule wake wa kwanza. Alisema kuwa juhudi zake kujaribu kushawishi mkewe arudi nyumbani hazikuwa zimefua dafu.

Hata hivyo juhudi za Ghost kumfikia Bi Jackline kwa simu hazikuzaa matunda licha yake  kujaribu kumpigia mara kadhaa.

Je, una maoni yepi kuhusiana na masaibu yaliyompata Shaban.