Faraja baada ya jamaa kupatanishwa na mamake wa kambo waliyekosana wakati dadake ambaye alikuwa atafutie kazi alipotea

Muhtasari

•Jamaa huyo alieleza kwamba baada ya juhudi za kumtafutia  kazi dadake aliyetambulisha kama Elizabeth kugonga mwamba mwanadada yule alitoweka asijulikane aliko hadi kufikia leo.

•Mamake Eliza alisema kwamba amemsamehe Kelvin kwani alikubali kukiri makosa yak

•Kelvin alieleza furaha yake baada ya kuweza kupatanishwa na mama yake wa kambo na akaapa kuanza juhudi za kumpata dada yake wa kambo.

Ghost na Gidi
Image: Studio

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kiengo cha Patanisho siku ya Jumatatu, Kelvin Babu alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mama yake wa kambo ambaye alimtambulisha kama Margaret.

Kelvin alidai kuwa walikosana na Bi Margaret mwezi Machi mwaka huu baada yake kukosa kufaulu kutafutia dadake wa kambo kazi kama alivyokuwa ameombwa na mamake.

Jamaa huyo alieleza kwamba baada ya juhudi za kumtafutia  kazi dadake aliyetambulisha kama Elizabeth kugonga mwamba mwanadada yule alitoweka asijulikane aliko hadi kufikia leo.

Kufuatia kutoweka kwa bintiye miezi sita iliyopita, Bi Margaret hajakuwa na uhusiano mzuri na mwanawe wa kambo.

"Aliniambia nitafutie dadake kazi. Akampatia nauli lakini baada ya dada kufunga safari hiyo kazi wakasema wamepata mtu. Huyo dadangu alipofika Nairobi baadae hakupatikana alipotea. Sijui ako wapi saa hii. Hata mama anasema hajui ako wapi.. Nilijaribu kupiga simu kwa dadangu mwingine lakini wakasema alifika tu kwa nyumba na akatoka." Kelvin alisimulia.

Cha kuogofya zaidi ni kuwa hakuna ripoti yoyote iliyopigwa kwa polisi kuhusiana na kupotea kwa mwanadada huyo.

"Hatuwezi jua mahali ako ju mama alinipigia simu akaniambia nikitaka vizuri niende nyumbani tuongee na yeye tutafute vile tutampata. Tayari alikuwa amefika kwa barabara akikuja wakati kazi ilikosekana" Kelvin aliambia Gidi.

 Bi Margaret alipopigiwa simu, Kelvin alipatiwa nafasi ya kumuomba mama yake wa kambo msamaha na kwa neema zake Mola wakaweza kuelewana. 

Mamake Eliza alisema kwamba amemsamehe Kelvin kwani alikubali kukiri makosa yake .

"Mi nimekusamehe imeisha. Mtu kama amekiri makosa yake nimemsamehe" Bi Margaret alisema.

Hata hivyo Margaret alisema kwamba bado hajafanikiwa kumwona dadake tangu mwezi Novemba mwaka uliopita ila ana matumaini kwamba bado ako hai.

Alisema kwamba kuna marafiki wa Eliza ambao walimfahamisha kwamba huwa wanamuona kupitia mtandao wa Facebook.

"Atakuja tu. Ako na Mungu. Mungu ndiye alimuweka kwa dunia atamleta. Kama ako ni sawa, kama ameenda ni sawa pia" Bi Margaret alisema.

Kelvin alieleza furaha yake baada ya kuweza kupatanishwa na mama yake wa kambo na akaapa kuanza juhudi za kumpata dada yake wa kambo.