Patanisho: "Nitatafuta pasta aniombee pepo ya kwenda kwa boma za watu itoke" Jamaa akubali kusalia nyumbani na mkewe

Muhtasari

•Karen alisema kuwa walikosana na mumewe mnamo mwezi Machi mwakani alipompatia onyo asiende kazi kwa maboma ya watu.

•Karen alidai kwamba huwa anaumia sana mumewe anapoenda mbali na kufuatia hayo hakumtaka aende.

•Anthony alisema kuwa alikuwa anaogopa kumwambia mkewe kuhusu mipango yake kwani yeye ni mkali

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, Bi Karen (30) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe Antony (40).

Karen alieleza kwamba wamekuwa kwa ndoa na Antony kwa kipindi cha miaka 7 na tayari wamebarikiwa na watoto watatu.

Mwanadada huyo alisema kuwa walikosana na mumewe mnamo mwezi Machi mwakani alipompatia onyo asiende kazi kwa maboma ya watu.

"Kuna wakati alienda kazi huko pande za Limuru mwezi wa tatu. Alifanya vizuri mwezi wa kwanza na wa pili, ilipofika mwezi wa sita nikaona pesa haitumwi. Baadae nikaona ananipigia simu eti nimtumie pesa. Nikamtumia ya kukula, credit lakini ikafika mahali pia mimi nikashindwa. Ikafika wakati akanipigia akaniambia kuwa sonko alikuwa amemfukuza kazini akaambiwa aende. Niliuza kuku nikamtumia nauli" Karen alisimulia.

Baada ya kutulia pale nyumbani kwa miezi kadhaa Anthony alianza kudai kuwa anataka kuenda kazi kwingine, hatua ambayo mkewe hakuifurahia.

Karen alidai kwamba huwa anaumia sana mumewe anapoenda mbali na kufuatia hayo hakumtaka aende.

"Mume wangu akiwa nje huwa naumia sana. Huwa nateseka maanake akifika huko huwa inabidi tena nimtumie pesa. Nimeuza kila kitu kwa nyumba nikamtumia" Alieleza Karen.

Alisema kwamba mumewe ana mazoea ya kukosana na mwajiri wake na kufukuzwa kazini kwa kuwa ana roho ndogo. 

Karen alitaka mumewe asalie pale nyumbani asiende kazi Eldoret ili ashughulikie kazi za kinyumbani.

Bwana Antony alipopigiwa simu alijitetea kwa kusema kuwa alipoteza kazi aliyokuwa anafanya Limuru baada ya mdosi wake kumuongeza kazi zingine tofauti na zile walikuwa wamekubaliana.

Alidai kwamba kazi mpya ambayo alikuwa ameitiwa ilikuwa tofauti na ile ambayo alikuwa amepoteza kwani ilikuwa ya kilimo biashara.

Antony alikuwa amepanga kufunga safari kuenda Eldoret siku ya Jumanne ila hakuwa amefahamisha mkewe. Alisema kuwa alikuwa anaogopa kumwambia mkewe kuhusu mipango yake kwani yeye ni mkali.

"Nilijua wewe ni wrong number siwezi kuambia mapema labda nikwambie nikitoka. Najua ningekwambia mara hiyo hiyo wewe huwezi kukubali" Anthony alisema.

Juhudi za Bi Karen na Gidi kushawishi Anthony kusalia nyumbani na familia yake ilifua dafu na wawili hao wakaelewa huku Anthony akikubali kufanya kazi za kilimo pale nyumbani.

"Kuanzia leo nataka nitafute mhubiri aniombee hiyo pepo ya kunisukuma niende kwa boma za watu nikiumia itoke. Hiyo pepo ikitoka najua mambo itakuwa sawa" Antony alisema.