Patanisho:"Nataka uniombee msamaha vizuri Wakenya wengi wasikie" Mwanadada alazimisha mumewe kumuomba msamaha hadharani

Muhtasari

•Dina alidai kwamba walikosana na mumewe kufuatia matusi mabaya na habari alizokuwa amepata kuwa  alikuwa na mwanamke mwingine.

•Dina hata hivyo alieleza kuwa mumewe tayari alikuwa amemuomba msamaha kufuatia hayo ila alitaka kupata hakikisho la kikweli ili aweze kurejea bila tashwishi yoyote.

•Joshua alifichua kuwa hapo awali mkewe alikuwa amemwagiza kusuluhisha mzozo wao kupitia kitengo cha Patanisho cha Radio Jambo ila kwa upande wake alitaka watafute suluhu kupitia majadiliano kati yao wenyewe.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha 'Gidi na Ghost  asubuhi' kitengo cha Patanisho, mwanadada aliyejitambulisha kama Dina (20) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe Joshua (27) ambaye walikosana mwezi Julai.

Dina alidai kwamba walikosana na mumewe kufuatia matusi mabaya na habari alizokuwa amepata kuwa  alikuwa na mwanamke mwingine.

"Kuna msichana ambaye niliambiwa ako na yeye. Nilipomuuliza akaniuliza kama nilimpata naye ama umeambiwa tu.Nikamwambia kwamba ningempata tu siku moja. Aliniambia kuwa hawakuwa wanazungumza na msichana yule ni kutembea tu pamoja. Akanitusi akaniambia ikiwa nataka kuolewa na mwanaume mwingine niende" Dina alisema.

Dina hata hivyo alieleza kuwa mumewe tayari alikuwa amemuomba msamaha kufuatia hayo ila alitaka kupata hakikisho la kikweli ili aweze kurejea bila tashwishi yoyote.

"Amekuwa akinipigia ananiambia nirudi lakini nimeona tu niiweke kwa Wakenya wengi wasikie. Ameniomba msamaha lakini nimeona aombe msamaha kwa Wakenya wengi ndio ata mimi nikuwe na roho ya kurudi vizuri" Dina aklisema.

Joshua alipopigiwa simu alisikika kushangazwa sana na habari kuwa kulikuwa na mtu ambaye alitaka kumuomba msamaha kwani kulingana naye, uhusiano kati yake na mkewe ulikuwa mzuri tu.

Joshua alidai kwamba tayari walikuwa wamesuluhisha mzozo ambao ulikuwepo na kusameheana.

"Unajua nilikuwa na msichana mwingine lakini tuliachana na yeye na nikakwambia kuwa sina maneno yoyote naye tena. Nimewahi kumpigia simu?? nilikueleza na ukakubali. Mimi sijawahi mpigia simu. Mimi huwa nakupigia simu na hata nakutumia pesa. Mimi sina shida na wewe, wewe ni mke wangu" Joshua aliambia mkewe.

Hata ingawa Dina alikubali kwamba walikuwa wamezungumzia mzozo ambao ulikuwepi kati yao alisisitiza kwamba alimtaka Joshua amuombe msamaha hadharani ili apate thibitisho kwamba alikuwa amejuta.

"Ile msamaha ulikuwa ukiniomba nataka kuisikia saa hii. Nataka uniombe hiyo msamaha vizuri ndio Wakenya wengi wasikie" Dina aliambia mumewe.

Joshua alifichua kuwa hapo awali mkewe alikuwa amemwagiza kusuluhisha mzozo wao kupitia kitengo cha Patanisho cha Radio Jambo ila kwa upande wake alitaka watafute suluhu kupitia majadiliano kati yao wenyewe.

"Nilimwambia ni afadhali tuelewane sisi wawili tu badala ya kuongea maneno mingi kwa watu. Nampenda ata akiniambia saa hii tuende anakotaka sina shida. Huyo ni mke wangu" Alisema Joshua.

Dina alisema kuwa aliridhishwa na hatua ya mumewe kumuomba msamaha hadharani na kusisitiza kwamba anampenda sana.

Je, una hisia zipi kuhusu Patanisho ya leo?