Patanisho: "Naomba urudi uendelee kuniosha, nimechafuka kabisa" Jamaa aliyefumaniwa na mpango wa kando asihi mkewe arudi

Muhtasari

•Solomon alidai kwamba walitengana  mwaka wa 2019  baada ya mkewe kumfumania na mpango wa kando kwake nyumbani.

•Solomon alieleza kuwa mpango wake wa kando alitoroka kupitia kwa dirisha wakati vita kati yake na mkewe ilikuwa imechacha.

•Millicent alieleza kwamba alipoenda kuchukua nguo zake alipata kuwa Solomon alikuwa ashaoa mke mwingine ambaye alimuonyesha madharau sana na kumfukuza.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Solomon Kisauna (35) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Millicent (29).

Solomon alidai kwamba walitengana  mwaka wa 2019  baada ya mkewe kumfumania na mpango wa kando kwake nyumbani.

Kabla ya hayo kutukia wawili hao walikuwa kwa ndoa kwa miaka miwili na kubarikiwa na mtoto mmoja tayari.

"Alinipata na mpango wa kando nyumbani. Tukaanza vita. Vile alinishinda nguvu na nikaanguka chini akachukua mtoto na kutoroka akaenda kwao" Solomon alisimulia.

Solomon alieleza kuwa mpango wake wa kando alitoroka kupitia kwa dirisha wakati vita kati yake na mkewe ilikuwa imechacha.

"Mpango wa kando alirukia kwa dirisha akaenda na akaniacha kama tunang'ang'ana na mke wangu.. tumekuwa tukiongea. Anasema ningoje kwanza apoe" Alieleza Solomon.

Alisema kwamba alikuwa amejuta sana baada ya kukamatwa na kuapa kuwa alikuwa amekoma tabia ya kuwa na mipango wa kando.

Millicent alipopigiwa simu alisimulia masaibu ambayo alipitia wakati alienda kuchukua mali yake kutoka kwa Solomon

Mwanadada huyo alieleza kwamba alipoenda kuchukua nguo zake alipata kuwa Solomon alikuwa ashaoa mke mwingine ambaye alimuonyesha madharau sana na kumfukuza.

"Nilirudi huko kuchukua nguo. Nilipata kama ameoa bibi mwingine.Vile niliomba nguo zangu hawakunipea, walininyima" Millicent alisimulia.

Solomon alifichua kwamba alikuwa anaishi na mpango wake wa kando wakati Millicent alienda kuchukua nguo zake. Hata hivyo, mwanadada huyo alimtema baadae na ndipo akaanza juhudi za kumshawishi mkewe arejee.

Alimsihi Millicent arudi nyumbani ili aendelee kumuonjesha mapenzi matamu ambayo alikuwa anampatia hapo awali kabla ya kukosana kama vile kumpapasa vizuri na kumuosha mwili.

"Nilikuwa nakupenda na sasa nataka tuendelee kupendana hivo. Nataka urudi tuendelee na maisha alafu unishike vile ulikuwa unanishika na unioshe. Saa hii ukiniona nimechafuka kabisa lakini wewe ulikuwa unaniosha" Solomon aliomba.

Millicent alisema kwamba alikuwa amemsamehea mumewe ila alihitaji muda wa mwaka mmoja kabla ya kufanya maamuzi ya kurejea.

"Nitarudi baadae kidogo. Anipatie muda nitulie kwanza. Nitarudi baada ya mwaka mmoja.. Nafanya kazi Nairobi ndio maana namwambia anipatie muda wa mwaka mmoja. Lazima anipatie muda wa mwaka mmoja nijue kama nitarudi"  Alisema Millicent.

Solomon alilalamika kuwa muda wa mwaka mmoja ulikuwa mrefu sana na kumuomba mkewe apunguze ila Milly alishikilia uamuzi wake. Hata hivyo alikubali kuendelea  kuwasiliana na Solomon ili kujadili mengi zaidi.