Patanisho: Jamaa atemwa kwa kukosa kuhudhuria matanga ya baba mkwe, adai kwamba mkewe amekuwa akiavya ujauzito

Muhtasari

•John alidai kwamba aligundua kuwa mkewe alikuwa amepata jamaa mwingine ambaye alimdanganya kwamba angelipa mahari na amuoe ila baadae akamfukuza.

•John alidai kwamba mkewe alikuwa na  mazoea ya  kuavya ujauzito kila anapoupata, madai ambayo alisema alielezwa na daktari wake.

•Mwanadada huyo alidai  kuwa mumewe alikuwa anamezea rafiki yake mate, jambo ambalo lilimkera zaidi.

Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama John Namahiva 30, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Josephine Awino 27.

John alidai kwamba mkewe aliondoka nyumbani akaenda kwao na kuacha kama amemuarifu kuwa ameenda matanga ya mjomba wake  ila baadae akagundua kuwa hakukuwa na matanga.

Alidai kwamba aligundua kuwa mkewe alikuwa amepata jamaa mwingine ambaye alimdanganya kwamba angelipa mahari na amuoe ila baadae akamfukuza.

"Mke wangu alisema anaenda matanga nikampa nauli.na akapanda gari akaenda ila baadae nikagundua kwamba haikuwa matanga. Nilipigia wazazi wake na ni kama kwamba walikuwa wananidanganya. Wazazi wake walisema kwamba ni ndugu ya babake aliyekufa ndipo nikampandisha gari akaenda, hadi saa hii hajarudi.

Anasema nimpatie miezi tisa ndio arudi. Nimefanya uchunguzi nikapata kumbe alikuwa amepata  jamaa mwingine akawadanganya kwamba yeye ni tajiri eti atalipa mahari akamchukua akampeleka Kisii ila saa hii naskia amemfukuza amerudi kwao. Dada yake ndiye ananiambia" John alisimulia.

Wawili hao wamekuwa kwa ndoa kwa miaka minane ila John bado hajalipa mahari na hawajapata mtoto yeyote pamoja.

John alimshutumu mkewe kuwa alikuwa na  mazoea ya  kuavya ujauzito kila anapoupata, madai ambayo alisema alielezwa na daktari wake.

"Hatujapata mtoto, huwa anatoa ujauzito kila anapopata. Daktari aliniambia kuwa kila anapopata ujauzit uwa anaenda analala na wanaume wengine. Kwa kuwa hizo damu hazisikizani huo ujauzito unatoka" John alidai.

Josephine alipopigiwa simu alisisitiza kwamba ni kweli alikuwa ameenda matanga ila hakuwa amerejea nyumbani kwake kwani alikuwa ameghadhabishwa na mumewe.

Alidai kuwa alisikitishwa na hatua ya mumewe kukosa kuhudhuria matanga ambayo alieleza kwamba yalikuwa ya babake na ndiposa hakuwa anataka kurudi.

"Matanga ilikuwa kwetu, ilikuwa ya babangu. Yeye hakukuja pamoja na familia yake ndiposa sijarudi bado. Aliniambia kuwa hana  pesa. Singeelewa kwani hata hakuambia familia yake. Sijui kama anataka nirudi ama anataka aje" Josephine alisema.

Alipuuzilia mbali madai ya John kuwa alikuwa amemtumia nauli ya kurejea nyumbani.

Josephine alilalamika kwamba licha ya kuwa wamekuwa pamoja kwa miaka nane, John huwa hazungumzi na familia yake kuhusiana na uhusiano wao.

Mwanadada huyo alidai  kuwa mumewe alikuwa anamezea rafiki yake mate, jambo ambalo lilimkera zaidi.

"Huyo rafiki yangu mwenye niliokota  kwa barabara anaitwa Eva nikamwambia akae kwa nyumba yangu. Tulikuwa tunaenda na yeye kanisani alafu tunarudi kwa nyumba. Kumbe ulikuwa unatamani Eva. Wakati niko kwa matanga wewe unaleta Eva kwa nyumba. Uliambia dadangu ati unatoa msongo wa mawazo na rafiki yangu" Josephine alimwambia John.

Alisema kuwa mumewe alikuwa na mazoea ya kutusi wazazi wake pamoja na dada yake.

Hata hivyo Josephine alimshauri John apige hatua ya kuenda kwa wazazi wake ili wajadiliane iwapo atarejea kwake.